Wataalamu wakiri kafyu ya mapema haina hata umuhimu

Wataalamu wakiri kafyu ya mapema haina hata umuhimu

Na CHARLES WASONGA

WATAALAMU wa afya wameonya kuhusu ongezeko la maambukizi ya corona katika maeneo ya Nairobi, Kiambu, Kajiado, Nakuru na Machakos kutokana na misongamano katika vituo vya matatu, wakazi wanapokimbia nyumbani kabla ya muda wa kafyu kuanza saa mbili za usiku.

Wataalamu hao wanaikosoa serikali, wakisema hatua ya kufunga kaunti hizo pamoja na kurefusha muda wa kafyu bila kuwapa wakazi chanjo na kuwapima Covid-19 kunahatarisha maisha zaidi.

“Hali hii ni hatari zaidi kwani serikali ilifaa kufunga kaunti hizo, kisha ianzishe upimaji corona na utoaji chanjo. Ilivyo sasa ni kwamba huenda hatua ya kufungwa kwa kaunti hizo na muda wa kafyu kuongezwa isilete nafuu kwa sababu tayari serikali inakabiliwa na uhaba wa chanjo,” akasema aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Lancet Kenya, Dkt Ahmed Kalebi.

Mkurugenzi Mkuu wa Amref, Dkt Githinji Gitahi anakubaliana na kauli hiyo, “Msongamano wa watu kwenye vituo vya matatu ni hatari hasa endapo utadumu kwa zaidi ya saa moja.”

“Kufungwa kwa kaunti hizo na kafyu hakukulenga kuzuia maambukizi inavyodhaniwa na wengi. Kulinuiwa kupunguza misongamano ya wagonjwa hospitalini,” akaeleza Dkt Githinji.

Lakini Kaimu Mkurugenzi wa Afya, Dkt Patrick Amoth anatetea hatua hizo akisema zimechangia kupungua kwa maambukizi.

“Sawa na kufungwa kwa baa na mikahawa, kafyu imeonekana kuzaa matunda. Msambao wa virusi vya corona ulikuwa juu zaidi wakati ambapo baa na mikahawa ilikuwa ikihudumu hadi saa tatu za usiku. Misongamano katika baa ni hatari zaidi kuliko ile ya vituo vya matatu kwa sababu kwenye baa ni nadra kwa walevi kuvaa barakoa,” Dkt Amoth akaambia Taifa Leo.

Wakenya wamekuwa na hofu ya kafyu kusababisha maambukizi zaidi, hasa kutokana na misongamano ya watu katika vituo vya matatu waking’ang’ania kwenda nyumbani kabla ya saa mbili jioni kafyu inapoanza.

Baadhi ya wakazi wa Nairobi waliozungumza na Taifa Leo walisema inawatesa kwa kuweka muda wa kafyu kuanza saa mbili za jioni ilhali wao hutoka kazini kuanzia saa kumi na moja jioni.

“Haya ni mateso tupu kwa sababu serikali imeamuru kafyu ianze mapema ilhali haijatoa amri kwa waajiri watuachilie mapema ilivyofanya mwaka jana. Mimi hufanya kazi Westlands na ninaishi mtaa wa Pipeline. Ninalazimika kuchelewa kufika kila siku kutokana na foleni ndefu katika kituo cha matatu,” akasema Bi Judith Oloo.

Kwa upande wake, John Irungu, mkazi wa eneo la Banana, Kiambu alielezea hofu ya kuambukizwa corona ikiwa serikali haitaongeza muda wa kafyu kuanza katika kaunti hizo tano.

“Hii kafyu ya kuanzia saa mbili usiku haitapunguza visa vya maambukizi ya corona kwa sababu matatu hujaza watu kupita kiasi kwa sababu kila mtu anataka kufika nyumbani,” akasema Bw Irungu ambaye ni mfanyakazi wa duka moja la jumla katikati mwa jiji.

You can share this post!

Hali mbaya ya uchumi yatia hofu Wakenya wengi –...

Biashara ya mitandaoni yawaletea Wakenya fursa mpya ya...