Habari za Kitaifa

Wataalamu wasema bangi haina madhara

January 15th, 2024 1 min read

NA MERCY CHELANGAT

MAMLAKA ya Kusimamia Vyakula na Dawa (FDA) imependekeza bangi kuorodheshwa upya kama dawa yenye kiwango cha chini cha madhara.

Hii ni baada ya wanasayansi kubaini kwamba bangi ina uwezo wa chini kutumiwa vibaya ikilinganishwa na dawa zingine za kulevya kama vile heroni.

Utafiti huo wa FDA, kamili kwa Kiingereza kama Food and Drug Administration, pia ulionyesha kuwa bangi ina kiwango cha chini kusababisha uzoefu kwa watumiaji wake.

FDA ni shirika lililoko chini ya Wizara ya Afya na Huduma kwa Binadamu, nchini Amerika.

Kwa sasa bangi imeorodheshwa kama dawa ya Kitengo cha Kwanza kinachosheheni dawa zenye kiwango cha juu zaidi cha kutumiwa vibaya na uwezo wa kusababisha watumiaji wake kushindwa kujitegemea kisaikolojia, au kimwili.

Watafiti hao wanataka bangi iwekwe katika Kitengo cha Tatu kinachosheheni uzoefu wa wastani hadi wa chini kimwili na kisaikolojia.

Mifano ya dawa za Kiwango cha Tatu ni: bidhaa zenye miligramu chini ya 90 kama vile Codeine kwa kila kipimo (Tylenol na Codeine), Ketamine, Steroids za Anabolic, na Testosterone.

Utafiti wa FDA pia umeainisha kiwango cha usaidizi wa Kisayansi bangi kutumika kwa minajili ya matibabu katika hospitali na kliniki kadha Amerika.

Aidha, bangi inaaminika kupunguza maumivu, kukabiliana na kero ya kutapika na kichefuchefu kinachotokana na matibabu ya Saratani – Chemotherapy, kulingana na watafiti.

Umauzi wa ikiwa bangi itaorodheshwa katika Kiwango cha Tatu, unasalia mikononi mwa Halmashauri ya Kimikakati Inayoshughulikia Masuala ya Dawa, ndiy Drug Enforcement Administration (DEA).

Nchini Kenya, bangi ni miongoni mwa dawa za kulevya zilizopigwa marufuku; kupandwa, kuuzwa na kutumika.