Habari MsetoSiasa

Wataalamu wataka marekebisho kabla ya 2022

April 21st, 2019 2 min read

Na RUSHDIE OUDIA

WATAALAMU katika fani mbalimbali wametaja ufisadi, gharama ya juu ya kuendesha uchaguzi na usimamizi mbaya kama baadhi ya masuala yanayochangia vurugu baada ya uchaguzi nchini na kuonya kwamba hali kama hiyo itashuhudiwa tena ikiwa mageuzi hayatafanyiwa IEBC.

Watalaamu hao, wanaojumuisha mawakili wa kikatiba na wanasiasa wanaonya kuwa endapo mageuzi makubwa hayatatekelezwa katika tume hiyo, Wakenya bado wataendelea kutilia shaka utendakazi wa tume hiyo siku zijazo.

Bw Wachira Maina, ambaye ni wakili wa masuala ya kikatiba, alisema marekebisho katika IEBC kwanza yanapasa kulenga suala la gharama ya kuendesha uchaguzi.

“Gharama ya demokrasia ni ghali sana nchini Kenya. Hii ni kwa sababu nchi hii huendesha uchaguzi ambao gharama yake ni mara 36 zaidi ya gharama ya shughuli hiyo nchini Rwanda,” akasema Bw Maina.

Ingawa kwa wastani gharama ya uchaguzi kwa mpiga kura mmoja ni Sh500, Bw Maina alisema kuwa uchaguzi mkuu wa 2017 uligharimu Sh2,890 kwa mpiga kura mmoja.

Rwanda ilitumia Sh150 kwa kila mpiga kura katika uchaguzi wa 2010, Uganda ilitumia Sh400 kwa mpiga kura mmoja mnamo 2016 na Tanzania ikatumia Sh516 kwa mpiga kura mmoja mnamo 2015.

Suala la gharama ya uchaguzi liliibuliwa siku ya mwisho ya mkutano wa madiwani uliondaliwa mjini Kisumu wataalamu walipojadili mabadiliko ambayo yanalenga kuimarisha mfumo wa uchaguzi nchini.

Bw Maina alisisitiza kuwa ipo haja ya udhibiti wa gharama ya uchaguzi.

“Ripoti kamili kuhusu gharama ya uchaguzi inapasa kuwasilishwa kila baada ya uchaguzi. Kwa mfano, nyingi ya vifaa vya kuendeshea uchaguzi vilivyonunuliwa wakati wa uchaguzi uliopita vilifeli kufanya kazi au vingine havikuwasilishwa. Huu ni ubadhirifu wa pesa za umma,” akasema Bw Maina.

Alisema wizi wa kura hutokea baada ya vifaa hivyo kufeli “kutokana na hitilafu za kimitambo au kwa kuvurugwa kimakusudi na maafisa wa kusimamia uchaguzi.

Bw Maina pia alisema hitilafu zilitokea katika uchaguzi uliopita kutokana na shida zilizotokea ndani ya IEBC, haswa miongoni mwa makamishna na maafisa wake.

“Shida kubwa ilikuwa ni ya kiusimamizi. IEBC haiwezi kutajwa kuwa huru ikiwa baadhi ya makamishna wanaegemea mirengo fulani au wakuu serikalini,” wakili huyo akasema.

Naye Dkt Collins Odotte ambaye ni mshauri katika masuala ya sheria za uchaguzi alisema gharama za uchaguzi nchini huwa juu kwa sababu ya ufisadi ndani ya IEBC.

“Gharama ya uchaguzi hupanda kwa sababu ya ufisadi uliokithiri katika idara ya ununuzi wa bidhaa na huduma na maamuzi yasiyofaa kuhusu vifaa hitajika,” akasema.

Dkt Odotte alionya serikali dhidi ya kutegemea sana matumizi ya mitambo ya teknolojia, ambayo hufeli siku ya uchaguzi.