Habari za Kitaifa

Wataalamu watumwa kuchunguza mipasuko ya kutisha Nakuru

May 15th, 2024 2 min read

NA JOSEPH OPENDA

SERIKALI imetuma wanajiolojia wakuu Nakuru kufanya uchunguzi wa kina baada ya mipasuko mikubwa a ardhi kuacha nyufa katika maeneo tofauti ya kaunti hiyo.

Mashimo yalitokea katika eneo la Kiambogo baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha hali ya taharuki katika vijiji vilivyo karibu.

Hivi majuzi maeneo ya Kaptembwo, Ngata na London nyufa kubwa katika mashamba ya watu.

Maeneo haya ni baadhi tu ya sehemu nyingi dhaifu katika eneo la Bonde la Ufa ambalo huanzia Upembe wa Afrika hadi Msumbiji.

Huko Kaptembwo, nyufa hizo ziliharibu nyumba zilizokuwa na wapangaji wiki jana huku huko Kiambogo, mashamba yakiachwa na nyufa kubwa.

Katibu wa Idara ya Serikali ya Madini Elijah Mwangi alisema tahadhari imetolewa kwa wenyeji wanaoishi katika maeneo yaliyoathiriwa.

Bw Mwangi alieleza kuwa kijiolojia, Kaunti ya Nakuru iko katika eneo linalokumbwa na aina mbalimbali za hatari za kijiografia ikiwa ni pamoja na mashimo, maporomoko ya ardhi na mitetemeko ya ardhi.

Hii inamaanisha kuwa kaunti iko katika eneo ambalo michakato ya kijiolojia inatokea sana chini ya ardhi.

Bw Mwangi alisema kwamba kaunti hiyo imewahi kuwa matukio ya sehemu za ardhi kuzama.

Matukio kama hivyo viripotiwa miaka ya 1972 na 1981 katika mzunguko ulio karibu na kituo cha petroli cha O’Jais.

Baada ya mvua ya El-Nino ya 1997, visa kama hivyo vitokea katika mtaa wa London.

Na mnamo 2004, tukio kama hilo lilitokea katika TimSales Compound na barabara ya Timber Mill.

Maeneo yenye udhaifu katika bonde la ufa yamekuwa na nyufa ambazo kwa kawaida hujaa majivu ya volkeno.

Lakini mvua zilizonyesha hivi majuzi zimezidisha hali hiyo kwa kusomba majivu hayo ya volkeno, na kuacha nyufa zikiwa wazi.

“Kwa sasa, shimo limeripotiwa katika eneo la Manyani kaunti ya Nakuru. Uchanganuzi wa awali wa hatari ya kijiografia unaonyesha mashimo hayo yanaweza kusababishwa na maji mengi ambayo mtiririko wake wa asili juu ya ardhi ulizuiwa na mitaro duni ya kuyaondoa. Maji yalitapakaa kwenye majivu ya volkeno, yakaungana na ya chini ya ardhi yaliyokuwepo awali na kusababisha kuzama kwa ardhi,” akasema Bw Mwangi.

Wakazi wa Nakuru katika maeneo hatari pia wametakiwa kuripoti dalili zozote za nyufa katika ardhi.

Mnamo 2018, sehemu ya barabara yenye shughuli nyingi ya Mai-Mahiu-Narok karibu na Suswa ilipasuka vipande viwili baada ya mvua kubwa kunyesha. Suswa iko sehemu ya chini ya Bonde la Ufa.