Habari Mseto

Watafunaji miraa walalamikia kodi ya juu

February 25th, 2019 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

WAFANYABIASHARA na watumiaji wa miraa kaunti ya Lamu wamelalamikia serikali ya kaunti hiyo kwa kuwatoza kodi ya juu ya bidhaa hiyo.

Wanabiashara hao wanasema katika siku za hivi karibuni, serikali ya kaunti imekuwa ikiwatoza fedha nyingi za kodi hasa wakati wanaposafirisha miraa hiyo Lamu, jambo ambalo linawanyima faida.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wanabiashara wa Miraa, Kaunti ya Lamu, Ibrahim Kamanja, wanabiashara hao walisema lori moja la miraa limekuwa likitozwa zaidi ya Sh 10,000 za kodi ili kufika Lamu.

Aliitaka serikali kuwapunguzia kodi hiyo ili kuwapa nafasi pia kupata faida wanapouza miraa.

Bw Kamanja alisema huenda biashara ya miraa ikafifia eneo hilo endapo kaunti haitabadili msimamo wake na kushukisha kiwango cha kodi kinachotozwa miraa.

“Unapotumia lori kusafirisha miraa kutoka Meru hadi Lamu utapoteza zaidi ya Sh 5000 barabarani. Kila kaunti tunayopitia wastahili kulipa Sh 1000. Kwa nini basi serikali ya kaunti ya Lamu isichukue hiyichukue Sh 10,000 badala ya Sh 1000 kama kaunti zingine? Wanatufanya hatupati faida tena kwenye biashara yetu. Washukishe kodi ili kuokoa biashara yetu,” akasema Bw Kamanja.

Peter Muriungi ambaye ni mmoja wa wanabiashara wa miraa, kaunti ya Lamu alisema idadi kubwa ya wauzaji miraa tayari wameacha biashara hiyo kutokana na kiwango cha juu cha kodi wanayotozwa.

Bw Muriungi alisema haoni sababu ya kaunti kuwatoza kiwango cha juu cha bidhaa hiyo, ikizingatiwa kuwa tayari wanabiashara wanapata taabu kusafirisha miraa kutoka Meru hadi Lamu.

“Baadhi yetu tayari tumesitisha kuendelea kuuza miraa Lamu kutokana na kodi ya juu. Huenda wanaweka kodi ya juu ili kutufungia nje hii biashara ya miraa. Wasikie kilio chetu na kushukisha bei au tugome,” akasema Bw Muriungi.

Bw Musa Dumilo alisema itakuwa vyema kwa kaunti kuwatoza wanabiashara wa miraa Sh 30 kwa siku badala ya kuwakata kodi ya Sh 10,000 kwa lori.

“Wanakataa kodi ya kawaida ya Sh 30 kwa kila mwanabiashara kwa siku. Wanashikilia kukata Sh 10,000 kwa kila lori na hiyo hatuikubali,” akasema Bw Dumilo.

Bi Zainab Abdalla ambaye ni mmoja wa watumiaji wa miraa kisiwani Lamu alisema kodi ya juu imechangia ongezeko la bei ya miraa kwa wanunuzi.

Awali kilo moja ya miraa ilikuwa ikiuzwa kwa kati ya Sh 1000 na Sh 1500.

Aidha tangu kaunti kuanza kuwatoza wanabiashara kodi ya juu ya miraa, kilo moja kwa sasa huuzwa kwa kati ya Sh 2000 na Sh 3000.

“Kaunti imepelekea miraa kuuzwa kwa bei ghali. Tunaandamana iwapo hawatashukisha kodi. Kwa nini watutese sisi wanabiashara na walaji wa miraaya miraa? Hatutakubali,” akasema Bi Abdalla.

Kwa upande wake aidha, Waziri wa Fedha na Masuala ya Bajeti wa Kaunti ya Lamu, Ahmed Hemed, alishikilia kuwa Kaunti ilikuwa haijaanzisha mpangilio wowote mpya wa utozaji kodi wa bidhaa hiyo.

Alisema mpangilio wa utozaji kodi wa miraa umekuweko zamani.

“Serikali ya kaunti haijabadili mpangilio wowote wa utozaji kodi kwa miraa. Tunafuata mpangilio uliokuweko zamani. Tulichofanya hasa ni kuongeza nguvu jinsi kodi inavyokusanywa eneo hili ili kuepuka ukwepaji wa kodi hiyo,” akasema Bw Hemed.

Mwisho