Makala

Watafunaji miwa wasababisha mende kusambaa kwa mabasi

February 7th, 2024 1 min read

NA RICHARD MAOSI

ABIRIA wenye mazoea ya kutupa kiholela maganda ya miwa na mabaki ya chakula ndani ya matatu na mabasi wamelaumiwa kwa kusababisha ongezeko la idadi ya mende na kunguni.

Haya ni kwa mujibu wa madereva na makondakta wanaotoa huduma za uchukuzi jijini Nairobi.

Waliozungumza na Taifa Leo walisema tabia hiyo chwara ya baadhi ya abiria imeharibia jina sacco na kampuni za mabasi na kusababisha baadhi ya wasafiri kutoroka magari hayo yao.

Kondakta Adrian Weche wa gari la uchukuzi wa umma kati ya Nairobi na Kitengela anasema amekuwa akisafisha gari kila baada ya siku mbili wala hajui kunguni wanatoka wapi.

“Tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha mazingira ya mabasi yetu ni mazuri lakini tabia chwara za baadhi ya abiria ziturudisha nyuma,” akasema Bw Weche.

Anasema hivi sasa wamiliki wa magari mengi wameweka kamera za CCTV ili kukabiliana na abiria wanaotupa uchafu kiholela.

Aidha wamiliki wameamua kuweka vibandiko vyenye ilani kali dhidi ya wale ambao watapatikana wakichafua magari hayo.

Kimojawapo cha vibandiko kinasema: “Kutapika ni Sh200.”

Pili Bw Weche anaungama kwamba sacco yao imeamua kuwachukuliwa hatua kali na hata kuwapiga faini abiria watakaopatikana na makosa hayo.

Katika takriban kila basi ambalo mwandishi ameabiri akiandaa makala hii, amebaini kuwa wamiliki wa mabasi kwa kawaida huwa wametenga sehemu maalum na majaa ya wasafiri kuweka taka hasa wale wa masafa marefu kuelekea mashambani.

Aidha baadhi ya wasafiri wanaobeba rundo la mizigo kwenye magunia na matandiko wamekuwa wakidhibitiwa vilivyo, baadhi ya mabasi yakidinda kubeba mizigo yao.

Hii ikiwa njia mojawapo ya kusaidia kupiga vita visa vya kusambaa kwa mende na kunguni.

Awali Taifa Leo iliripoti visa ambapo mabasi ya Nairobi yanatuhumumiwa kwa kuwasambazia wasafiri kunguni.

Maeneo yaliyoorodheshwa ni Rongai, Githurai, Kangemi na mabasi ya kuelekea Kitengela kupitia Mlolongo.