Habari Mseto

Watahiniwa 2 wafariki KCSE, mwalimu afa akisahihisha KCPE

November 14th, 2019 1 min read

Na WAANDISHI WETU

Watahiniwa wawili wamefariki kwenye Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) unaoendelea huku mwalimu akifariki wakati akisahihisha Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) jijini Nairobi.

Kulingana na mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) Dkt John Onsati, mwalimu huyo alitambuliwa kama Bw Robert Kiua Muindi.

Alikuwa akifunza katika Shule ya Msingi ya Tusunini katika Kaunti ya Makueni.

“Mwalimu aliugua ghafla katika kituo kimoja cha kusahihishia mitihani jijini Nairobi na akakimbizwa katika Hospitali ya Misheni ya PCEA Kikuyu alikofariki,” akasema Dkt Onsati.Katika Kaunti ya Homa Bay, mtahiniwa wa KCSE alifariki wakati akifanya mtihani huo katika Shule ya Upili ya Nyawita kutokana na upungufu wa damu.

Mwathiriwa alitambuliwa kama Belinda Atieno mwenye umri wa miaka 20. Alifariki mnamo Jumanne katika Hospitali ya Matata iliyo katika mji wa Oyugis.

Mtahiniwa huyo alikuwa akifanyia mtihani wake katika kituo cha afya kilicho karibu wakati hali yake ilipozorota.

Katika Kaunti ya Nakuru, familia moja katika kijiji cha Majani Mingi, eneo la Rongai inaomboleza baada ya mwana wao kufariki alipomaliza kufanya Karatasi ya tatu ya Somo la Kemia.

Mtahiniwa huyo alitambuliwa kama Victor Kiptoo mwenye umri wa miaka 18 kutoka Shule ya Upili ya Mseto ya Barina.

Alifariki Jumatatu akipelekwa hospitalini.Chanzo cha kifo chake bado hakijabainika, ingawa familia yake inasema kuwa kuna uwezekano kilitokana na kemikali walizotumia kwenye mtihani huo.