Habari

Watahiniwa KCPE kujua shule za upili kabla Krismasi

November 1st, 2019 1 min read

Na FAITH NYAMAI

WANAFUNZI waliofanya mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) mwaka 2019 watajua shule za sekondari ambazo watateuliwa kujiunga nazo kabla ya Krismasi, Waziri wa Elimu Profesa George Magoha amesema.

Akihutubia wanahabari katika shule ya msingi ya Ayany, Nairobi alikokagua mtihani huo uliokamilika Alhamisi ulivyoendeshwa, Profesa Magoha alisema usahihishaji utaanza mara moja na matokeo kutangazwa kabla ya Krismasi.

“Watoto wataweza kujua shule ambazo watajiunga nazo kwa kidato cha kwanza punde tu baada ya matokeo kutolewa ili wazazi wao wapate kuwaandaa,” alisema.

Alisema kulikuwa na visa vya kujaribu kuiba mtihani huo katika kaunti tatu.

Visa hivyo viliripotiwa Nyandarua, Pokot Magharibi na Garissa.

Profesa Magoha alisema Tume ya Kuwaajiri Walimu tayari imewachukulia hatua walimu waliohusika na uovu huo.

“Mimi binafsi sina huruma kwa yeyote anayechagua kuhusika na wizi wa mtihani na sheria itachukua mkondo wake kikamilifu,” alisema.

Profesa Magoha alisema wakati wa kusahihisha ikigunduliwa kwamba kuna vituo vingine vilivyohusika na udaganyifu, hatua kali za kisheria zitachukuliwa wahusika.

Hata hivyo, waziri alisema Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) limekuwa likijitahidi kumaliza udanganyifu kwenye mitihani katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

“Idadi ya visa vya udaganyifu imepungua mno,” alisema.

Alisema hakuna karatasi ya mtihani iliyoibwa kwenye mtihani wa mwaka kuu kwa sababu watahiniwa wote walishuhudia kufunguliwa kwa karatasi zote kabla ya kuanza mtihani na kwamba, mwaka huu, kila mmoja wao atapata alama inayomfaa.

Mwaka huu kulikuwa na changamoto tele miongoni mwao mvua kubwa iliyosababisha mito kufurika na barabara kuharibika kote nchini.

“Tulipiku changamoto za hali ya hewa kuhakikisha watoto wote wanafanya mtihani bila kuchelewa,” alisema.

Profesa Magoha pia alimshukuru Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kwa kutoa msaada uliohitajika kufanikisha mtihani huo.

Vituo 20 vilifanya mtihani vikiwa vimechelewa siku ya kwanza na ya pili karatasi zilipochelewa kutokana na hali mbaya ya hewa.