Watahiniwa wahamishwa kwa ndege ya KDF msituni Boni

Watahiniwa wahamishwa kwa ndege ya KDF msituni Boni

NA WAANDISHI WETU

WAKATI wanafunzi wapatao milioni 2.5 walipokuwa wakijiandaa kwa mitihani yao ya kitaifa ya Gredi 6 na Darasa la Nane jana Jumatatu, watahiniwa kutoka shule zilizo msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu, walikuwa wanapitia hali isiyo ya kawaida.

Safari yao ya elimu haijawa rahisi. Imekuwa ikitatizwa mara kwa mara kwa sababu za kiusalama.

Boni hutatizika kwa mashambulio ya kigaidi ambayo hufanya shule kufungwa kwa muda, huku walimu wengine wakihama kwa kuhofia usalama wao.

Ili kuzuia mitihani hiyo muhimu kutatizwa, serikali iliamua kutuma wanajeshi wa KDF kuwasafirisha watahiniwa 28 wa Gredi ya 6 kwa ndege hadi Shule ya Upili ya Faza.

Watahiniwa wa Darasa la Nane walikuwa wamehamishwa awali kusomea katika Shule ya Mokowe Arid Zone ambayo ni ya bweni, iliyo Lamu Magharibi.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia alisema walimu wanane pia walisafirishwa pamoja na wanafunzi hao na wataishi Shule ya Upili ya Faza hadi mtihani utakapokamilika.

“Tuko imara kuhakikisha mtihani unafanywa bila usumbufu wowote wa kiusalama,” akasema Bw Macharia.

Mkurugenzi wa Elimu Lamu, Bw Joshua Kaaga, aliwashauri wasimamizi wa mitihani na maafisa wa usalama kuwa macho na kuripoti kisa chochote kisicho cha kawaida ili hatua mwafaka zichukuliwe haraka.

Katika Kaunti ya Tana River, ilibainika takriban wanafunzi 7,000 hawako shuleni katika shule za msingi na upili.

Kamishna wa Kaunti hiyo, Bw Thomas Sankei, alisema zaidi ya wanafunzi 5,000 waliotarajiwa kufanya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) hawajulikani waliko.

Vilevile, takriban wanafunzi 2,000 waliokuwa wamejiunga na Kidato cha Kwanza miaka minne iliyopita, hawako kwenye orodha ya waliosajiliwa kufanya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE).

Kwingineko Kwale, walimu wa watahiniwa walionywa dhidi ya wizi wa mitihani.

Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Kwale, Bw Martin Cheruiyot, alionya kuwa walimu watakaopatikana wakichangia udanganyifu wa mitihani wataachishwa kazi na kushtakiwa.

Kwa upande mwingine, alisema watahiniwa hao wanaweza kukosa matokeo yao iwapo itababainika kutenda udanganyifu wakati wa mtihani.

Katika eneo la Pwani, jumla ya watahiniwa 110,807 walisajiliwa kufanya KCPE huku 127,573 wakisajiliwa kufanya mtihani wa kitaifa wa Gredi ya 6.

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Mpango wa kuwapa machifu bunduki...

Korti yazima serikali kuagiza mahindi tata

T L