Habari Mseto

Wataka kampuni ya mawe ifungwe

January 15th, 2020 2 min read

NA LAWRENCE ONGARO

FAMILIA ya wakazi 500 katika kijiji cha Mukunike, Thika Mashariki wanaiomba serikali kufunga kampuni moja ya kusaga mawe.

Wakazi hao wanalalamika kwa kusema ya kwamba kampuni hiyo ya kichina imekuwa kero kubwa karibu na makazi yao kwa kusababisha vumbi na mawe kuruka hadi manyumbani mwao.

Kampuni hiyo ya Sinohydro Corporation husaga mawe ambayo hugeuzwa kama kokoto ya kujenga nyumba na kazi hiyo huendeshwa masaa 24 mfululizo.

Wakazi hao walizidi kuteta ya kwamba kwa muda mrefu sasa maradhi ya kifua , kuumwa na kichwa yamekua hayaishi mwilini mwao na sasa imeathiri kabisa wakaazi wa kijiji hicho.

Bi Jane Njeri Njoroge alisema mnamo Jumatatu jioni jiwe kubwa liliruka kutoka katika kiwanda hicho na kubomoa mabati ya nyumba yake ambapo kama siyo uwezo wa Mungu angekuwa maiti.

“Jiwe hilo kubwa liliruka kwa kishindo na kwa bahati nzuri ilitua kando ya kitanda changu cha kulala. Mimi nilishtuka kusikia sauti kubwa kumbe ilikuwa ni jiwe hilo,” alisema Bi Njoroge.

Bi Maria Mumbua ni mkazi mwingine ambaye anasema pia alinusurika kifo wakati jiwe lingine liliangukia kando ya mguu wake akiwa ndani ya nyumba yake.

“Mimi sikuamini macho yangu kwani nilishtuka bati la nyumba yangu limebomoka na jiwe kuniangukia kwa kishindo. lakini ni bahati ya mwenyezi Mungu kwani ningevunjika mguu,” alisema Bi Mumbua.

Alisema kanisa moja lililo karibu na eneo hilo na shule ya St Mary Academy zimeathirika na vumbi hiyo ambayo imeleta shida za kiafya kwa wengi.

Alisema licha ya wakazi wa hapa kulalamikia kitendo hicho bado hakuna yeyote amewajali kwa kuwapa matumaini .

Bi Mumbua alisema alihamia eneo la kijiji hicho hivi majuzi baada ya kuhama kutoka Gichiiki eneo za Kilimambogo wakati kulitokea mafuriko.

“Bado ninaendelea kupata shida za hapa na pale. Mimji na familia yangu hatuna amani na hatujui ni lipi tutafanya baada ya masaibu hayo yote,” alisema Bi Mumbua na kuongeza serikali inastahili kuingilia kati na kuondoa kampuni hiyo eneo hili.

Diwani (MCA), wa eneo la Ngoliba Bw Joachim Mwangi, alisema atafanya juhudi kuona ya kwamba anawasilisha mswada katika bunge la Kaunti ya Kiambu ili kuona ya kwamba matakwa ya wakazi hao inazingatiwa kwanza.

“Nitafanya juhudi kuona ya kwamba kamati ya mazingira inashughulikia jambo hilo  haraka iwezekanavyo ili wakazi hao wasiendelee kuumia,” alisema Bw Mwangi.

Alisema yeye kama kiongozi wa eneo hilo hatakubali kuona wawekezaji wachache wakijitajirisha huku wananchi wakiumia.