Habari za Kitaifa

Viongozi wa kidini wataka muguka kupigwa marufuku kote nchini

May 24th, 2024 2 min read

NA TITUS OMINDE

VIONGOZI wa kidini kutoka North Rift wanataka serikali kuharamisha biashara ya muguka na miraa.

Kwa pamoja, wanataka mabunge ya kaunti zote kutunga sheria za kuharamisha biashara hiyo ili kuwalinda vijana dhidi ya athari za utumizi wa dawa za kulevya.

Wakiongozwa na Baraza la Maimamu na Wahubiri Nchini (CIPK) wanataka muguka na miraa kuwa kati ya dawa zilizopigwa marufuku ili kulinda vijana dhidi ya athari za dawa za kulevya nchini.

“Matumizi ya miraa na mugukaa ndio huchochea matumizi ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na unywaji wa pombe ya gharama ya chini ya ubora wa kutiliwa sahaka na mihadarati kama heroini na bangi. Biashara hiyo inafaa kuharamishwa,” alisema Sheikh Abubakar Bini, ambaye ni Mwenyekiti wa CIPK tawi la North Rift.

Waliunga mkono msukumo wa Seneta Maalum Prof Margaret Kamar wa kutambulisha mazao mengine ya biashara kama chai na kahawa kuchukua nafasi ya miraa na muguka.

“Vijana wengi wanaotumia miraa na muguka hutumbukia kwa uraibu wa kunywa pombe na kuvuta sigara na vilevile bangi na mihadarati mingine inayoleta madhara kwa jamii,” akaongeza Bw Bini.

Naye Sheikh Rashid Kiplagat Songok alisema vita dhidi ya utumizi wa dawa za kulevya havihitaji kuingizwa siasa.

“Vita hivi vinahitaji juhudi za pamoja za viongozi wote wakiwemo wabunge. Ni wakati mwafaka wa Nacada kuorodhesha miraa na muguka miongoni mwa dawa zilizopigwa marufuku,” alisema Sheikh Songok.

Kulingana na viongozi hao, miraa na muguka huuzwa katika maeneo ya wazi ikiwa ni pamoja na vituo vya mabasi na makazi na kurahisisha vijana kununua bidhaa hiyo kwa bei ya chini ya Sh50.

“Kuna uhusiano wa karibu kati ya vijana wanaokula miraa na unywaji wa pombe haramu hadi usiku wa manane na kujihusisha katika vitendo vya uhalifu ikiwa ni pamoja na wizi wa kimabavu,” alisema Ali Juma wa kutoka msikiti wa Kipkaren.

Muguka ni nafuu kuliko miraa na bidhaa hiyo inazidi kupata umaarufu miongoni mwa vijana huku maduka kadhaa yakianzishwa katika maeneo ya wazi, masoko na maeneo ya makazi.

Tayari Serikali ya Kaunti ya Mombasa imepiga marufuku usafirishaji na matumizi ya muguka ndani ya kaunti hiyo.

Gavana Abdulswamad Nassir, alitoa amri kwamba maduka yote yanayouza bidhaa hiyo yafungwe mara moja, akataka maafisa wa usalama wa kaunti pia wazuie magari yatakayopatikana yakijaribu kusafirisha muguka katika jiji hilo.

Hatua hii inajiri wakati ambapo utawala wa kaunti hiyo unazidi kuchukua hatua kali za kudhibiti utafunaji muguka na miraa, ikisemekana uhuru uliopo umefanya watoto wa shule kujiingiza katika uraibu huo.

Nayo Kaunti ya Kilifi mnamo Ijumaa ilijitokeza kaunti ya pili kupiga marufuku uuzaji wa muguka. Gavana Gideon Mung’aro alisema magari yanayosafirisha muguka hayataruhusiwa kuingia kaunti hiyo. Haya yanajiri siku chache baada ya Mombasa kutangaza marufuku hayo.