Habari MsetoSiasa

Wataka Rais atatue suala la mizigo SGR

August 15th, 2019 1 min read

Na MOHAMED AHMED

BARAZA la Maimamu na Wahubiri nchini (CIPK) limemuomba Rais Uhuru Kenyatta aingilie kati suala la watu kulazimishwa kusafirisha mizigo kwa njia ya reli.

Viongozi hao wa Kiislamu walisema kuwa licha ya kusitishwa kwa agizo hilo lililokuwa limetolewa na Mamlaka ya Ushuru Nchini (KRA) pamoja na usimamizi wa bandari (KPA), hali ya biashara imedorora.

Akizungumza katika kikao na wanahabari kwa niaba ya baraza hilo, mweka hazina, Sheikh Hassan Omar alisema kuwa tayari kuna kampuni za uchukuzi ambazo zimeanza kufuta wafanyakazi wake.

“Kwa sababu ya hali hii tunamuomba Rais Kenyatta aingilie kati na kusimamisha yeye binafsi agizo hilo. Serikali haipaswi kufanya SGR kuwa in lazima kwa wafanyabiashara,” akasema Sheikh Omar.

Kiongozi huyo alisema si sawa kwa serikali kuwatesa raia wake wanaojitafutia riziki kwa njia halali, na kutoa mfano wa baadhi ya wafanyabiashara wanaoteseka kwa sababu ya kusafirisha mizigo yao Nairobi.

Alisema kuwa maeneo ya kuegesha makasha jijini Mombasa yameachwa matupu kwani makasha mengi yamepelekwa Nairobi kwa lazima.

“Wengine wanalazimika kufuata makasha yao Nairobi na kupata hasara kwani wakati mwingine baadhi ya mizigo huwa imepangiwa kushukishwa Mombasa,” akasema.

Aliongeza kuwa serikali inapaswa kuweka wazi ushindani wa kibiashara na sio kuwalazimisha kutumia SGR.

Wakati huo huo, mwenyekiti wa CIPK kaunti ya Mombasa Sheikh Mohammed Shaaban, alisema kuwa familia nyingi zinategemea bandari ya Mombasa na baadhi ya hatua huenda zikaleta umaskini.