Habari Mseto

Wataka serikali iboreshe utaratibu wa kuwafidia wenye vipande vya ardhi chini ya miradi ya serikali

September 13th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

WAMILIKI wa vipande vya ardhi ambao wameathirika na miradi ya serikali watalazimika kungoja kwa muda mrefu iwapo sheria mpya ya kulipa fidia itatekelezwa.

Kulingana na sheria zilizowekwa chini ya Land Value Amendment Act 2019, itachukua mwaka mmoja au zaidi kulipwa fidia iwapo serikali itatumia kipande cha mmiliki ardhi kwa miradi yake.

Hata hivyo, masorovea chini ya Taasisi ya Masoroveya Kenya (ISK), wametaka sheria hiyo kuangaliwa upya wakidai kuwa haizingatii usawa na haki.

“Kulipwa fidia kwa vipande vya ardhi kunafaa kuzingatia hali ya uchumi na bei ya wakati huo ambayo haijapitwa na wakati ili kuhakikisha kuwa walioathirika hawatapata hasara,” amesema Rais wa ISK Bw Abraham Samoei.

Bw Samoei ameilaumu serikali kwa kuchukua muda mrefu kuwafidia walioathirika licha ya kuwa na bajeti.

Baadhi ya wanachama wa Taasisi ya Masoroveya Kenya (ISK) wakati waliandaa kikao na wanahabari jijini Nairobi. Picha/ Magdalene Wanja

“Serikali ina bajeti ya kufanya miradi pamoja na ile ya kulipa fidia na hivyo si haki kuwafanya wananchi kuteseka bila mahali mbadala baada ya kuvichukua vipande vyao vya ardhi,” akasema Bw Samoei.

ISK pia imelaumu serikali kwa kuunda mahakama (tribunal) ambayo haina washauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya ardhi kama vile wakadiriaji thamani (valuers).

“Hii inaonyesha kwamba mahakama hiyo haina uwezo wa kufanya kazi yake kwa ukamilifu na iwapo marekebisho hayatafanywa, itakuwa ni utumizi mbaya wa fedha za umma,” alisema Bw Samoei.