HabariSiasa

Wataka Uhuru aeleze ikiwa ni yeye humpa Ruto hela za michango

September 4th, 2019 1 min read

Na JOSEPH WANGUI

WABUNGE wa mrengo wa ‘Kieleweke’ kutoka Mlima Kenya wanaitaka Ikulu kueleza ikiwa Rais Uhuru Kenyatta huwa anampa Naibu Rais William Ruto pesa za kutoa kwenye michango ya makanisa anayohudhuria.

Wikendi iliyopita, Dkt Ruto alitoa jumla ya Sh7.5 milioni kwenye harambee za makanisa manne katika kaunti za Nyeri na Kirinyaga, akisema Sh2 milioni zilikuwa mchango kutoka kwa Rais Kenyatta.

Mjini Nyeri, alitoa Sh3 milioni kwa kanisa la ACK St Paul’s Kariki, Othaya, Sh2 milioni zikiwa mchango wake binafsi huku Sh1 milioni zikiwa mchango wa Rais Kenyatta.

Vile vile, alitoa Sh1 milioni kwa kanisa la AIPCA Narumoru katika eneo la Kieni.

Katika Kaunti ya Kirinyaga, alitoa Sh3 milioni kwa Kanisa la Katoliki la Parokia ya Kangaita, mjini Kerugoya. Kwenye mchango huo, Sh2 milioni zilikuwa mchango wake binafsi, huku Sh1 milioni zikiwa mchango kutoka kwa Rais Kenyatta. Baada ya hapo, alielekea katika Kanisa la Full Gospel Gichugu, alikotoa Sh500,000.

Wakiongozwa na Mbunge Maalum Maina Kamanda, wanasiasa hao walisema Rais Kenyatta anapaswa kueleza ikiwa ndiye huwa anatoa michango hiyo kama vile Dkt Ruto amekuwa akidai.

“Uhuru anapaswa kutwambia ikiwa yeye ndiye amekuwa akimtuma Dkt Ruto na michango ya Sh1 milioni katika kila hafla ya kuchangisha pesa anayohudhuria. Sababu kuu ni kwamba amegeuza makanisa katika eneo la Kati kuwa majukwaa ya kufanyia siasa,” akasema Bw Kamanda, ambaye amekuwa akiongoza kampeni dhidi ya Dkt Ruto.

Kulingana na mwanasiasa huyo mkongwe, Dkt Ruto hatapata uungwaji mkono wowote kwa kumpinga Rais Kenyatta, hasa kwenye mipango yake kama Jopo la Maridhano (BBI).

Kwenye ziara yake katika Kaunti ya Nyeri, Dkt Ruto alitaja jopo hilo kama upotezaji muda.

“Eneo la Kati halitadanganyika kumfuata. Tuko kila mahali tukijenga daraja la maelewano,” akasema Bw Kamanda.

Kauli yake iliungwa mkono na wabunge Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini) na Maoka Maore (Igembe Kaskazini).