Habari Mseto

Wataka waziri aagizwe kutoa mkataba wa SGR

February 19th, 2020 2 min read

Na PHILIP MUYANGA

WACHUKUZI wanataka waziri wa Uchukuzi James Macharia aagizwe kuweka kortini mkataba wa makubaliano baina ya serikali ya Kenya na ile ya Uchina, kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Chini ya mwavuli wa Kenya Transporters Association (KTA), wachukuzi hao wanasema kuwa kesi walioiwasilisha mahakamani inauliza maswali kuhusu agizo la Halmashauri ya Bandari nchini (KPA) na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA), likitaka mizigo yote kutoka nchi za nje kupitia bandari ya Mombasa kusafirishwa hadi Nairobi kupitia SGR pekee.

Wanasema kuwa kulingana na maelezo kuhusu agizo hilo, itadhihirika wazi kuwa agizo hilo liliwekwa ili kutengeneza pesa kupitia shughuli za uchukuzi.

Wachukuzi hao wanasema kuwa wanaamini kuwa usafirishaji wa makasha kwa kutumia SGR ni kutengeneza pesa ili zitumike kulipa mkopo uliopeanwa kwa serikali na China kwa ajili ya kugharimia mradi wa SGR.

“Ni muhimu kuangalia agizo hilo kuanzia msingi wake ukiwa ni mkataba wa makubaliano wa ujenzi wa SGR nchini na serikali ya Uchina,” wachukuzi hao walisema.

Waliongeza kuwa ni muhimu kuangalia mkataba wa makubaliano ili kupatia nafasi wahusika katika kesi kujieleza kuhusiana na maelezo yaliyotolewa.

Wachukuzi hao wanasema kuwa agizo la KPA na KRA lina athari kubwa kwa uchumi wa kitaifa ndiposa maswali ambayo yanahusika na mkataba wa makubaliano ni muhimu kwao.

“Kwa kuwa mkataba wa makubaliano haufahamiki na umma, itakuwa muhimu na haki iwapo mahakama itaagiza kuwa mkataba wa makubaliano upeanwe kwa wachukuzi na mahakama,” waliongeza.

KTA inasema kuwa kutolewa kwa mkataba huo wa makubaliano kutasaidia mahakama kupata malengo bora huku ikitilia maanani ni jambo muhimu katika kuamua kesi hiyo.

Katika kesi yao, wachukuzi hao wanataka wawe huru kuchagua mbinu ya usafirishaji wa mizigo yao wanapoiagiza kutoka nje.

Wachukuzi hao wamewashtaki KPA,KRA,KRC,waziri wa uchukuzi Bw Macharia na halmashauri ya kudhibiti ushindani wa kibiashara biashara nchini (CAK).

KTA inasema kuwa badala ya kuimarisha maelezo kuhusu utumiaji wa SGR,serikali imezuia wachukuzi kufanya uamuzi wao kuhusiana na njia ya usafirishija mizigo ambayo ni mwafaka kwao.

Wachukuzi hao wanasema kuwa wanaoleta mizigo nchini wanalindwa kikatiba kuhusiana na chaguo lao la usafirishaji wa mzigo sehemu yoyote nchini.

KTA inasema kuwa maagizo yaliyotolewa na KPA na KRA kwa njia ifaayo shirika la reli nchini hayakuhusisha mchango wa wananchi.

“Serikali inafanya kana kwamba SGR ndio muundo msingi pekee ambao imeekeza nchini na kusahau kuwa muundo msingi wa barabara na kampuni za uchukuzi zimekuwa sehemu kuu ya kujipatia raslimali,” KTA walisema katika stakabadhi za kesi yao.