Habari

'Watakaorejesha bunduki wanazomiliki kinyume cha sheria kufikia mwisho wa Septemba hawataadhibiwa'

September 21st, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imewataka Wakenya wanaomiliki bunduki kinyume cha sheria kutumia muda wa msamaha wa mwezi mmoja uliotolewa kuzirejesha.

Mkurugenzi wa Shirika la Kitaifa la Kudhibiti Matumizi ya Silaha (KNFP) Mohamed Amin amesema Jumamosi uchunguzi ulioendeshwa na shirika la Africa Amnesty umefichua kuwa Kenya ina zaidi ya bunduki 600,000 mikononi mwa watu kinyume cha sheria.

Bw Amin ameahidi kwamba wale ambao watarejesha bunduki haramu kabla ya Septemba 30 hawatachulikuwa hatua zozote za kisheria.

“Uchunguzi wa hivi majuzi imefichua kuwa kati ya bunduki 550,000 na 650,000 ziko mikononi mwa raia kinyume cha sheria. Silaha hizi zinafaa kuerejeshwa kwa serikali ili zisitumiwe kutekeleza uhalifu,” akasema Bw Amin.

“Serikali imeweka mikakati ya kutwaa silaha haramu. Kwa hivyo, wale watakaorejesha bunduki hizo kabla ya Septemba 30, watasamehewa katika kipindi hiki cha msamaha kilichoanza Septemba 1,” akawaambia wanahabari katika mkahawa wa Serena, Nairobi.

Bw Amin amesema wenye bunduki hizo haramu wanapaswa kuzisalimisha kwa vituo vya polisi vya karibu, kwa viongozi wa kidini au viongozi wa kijamii bila kuhofia kukamatwa.

Mkurugenzi huyo amesema serikali itaharibu silaha hizo – zitakazokuwa zimesalimishwa – hadharani mwishoni mwa mwaka 2019.

“Ulimwengu utafurahia amani ya kudumu ikiwa silaha haramu zitatwaliwa kutoka kwa watu wanaozimiliki,” Bw Amin akasema.

Wakati huu serikali inahodhi zaidi ya bunduki 8,000 zinazomilikiwa kiharamu na zilizotwaliwa kutoka kwa wananchi.

Uamuzi wa viongozi

Hatua ya serikali ya kuwaruhusu raia kusalimisha bunduki haramu katika mwezi huu wa Septemba inaenda sambamba na Uamuzi wa Marais wa Mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).

Marais hao 52 walitangaza Septemba kuwa mwezi wa kusalimishwa kwa silaha zinazomilikiwa na wananchi kinyume cha sheria.

Mnamo Februari mwaka huu serikali ilianzisha mchakato wa kuwapiga msasa upya wenye leseni ya kumiliki bunduki kuhakikisha kuwa ni wale walio na ujuzi wa kutumia silaha hizo pekee wanapewa leseni mpya.

Serikali ilisema shughuli hiyo pia ililenga kuhakikisha kuwa raia wenye leseni za kumiliki bunduki hizo wanafuata kanuni mpya za matumizi yazo zilizoanzishwa na Wizara ya Usalama wa Ndani.