Habari

Watakubali handisheki yao?

March 16th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, walipozika tofauti zao za kisiasa na kuungana mwaka 2018, matarajio ya wengi yalikuwa kwamba uhasama wa kisiasa baina ya vigogo wa kisiasa nchini ungemalizika.

Hata hivyo, tofauti kati ya Naibu Rais William Ruto na Bw Odinga zimekuwa zkiongezeka kila uchao. Swali ni, wawili hao wataamua kuzika tofauti zao na kufanya kazi pamoja?

Ijumaa kiwa Kisii, Dkt Ruto aliendelea kumlaumu Bw Odinga na washirika wake wa kisiasa kwa kupanga njama ili afukuzwe katika chama cha Jubilee.

Alisema akiwa mwanzilishi wa chama cha Jubilee ameona dalili kwamba Bw Odinga anaendelea kukivunja. Dkt Ruto aliapa kukabiliana na wapinzani wake vikali na kuapa kutokubali mgawanyiko katika chama tawala.

Dkt Ruto amekuwa akimlaumu waziri mkuu wa zamani kwa kuvuruga serikali na kutumia muafaka wake na Rais kuwahangaisha baadhi ya watu.

Wafuasi wa viongozi hao wamekuwa wakilumbana katika mikutano ya umma, wale wa Naibu Rais wakidai kuna mpango wa kumzuia kiongozi wao kuingia ikulu kwenye uchaguzi wa 2022.

Wawili hao wamekaidi ushauri wa viongozi wa kidini wanaowataka wasalimiane na kusubiri 2022 washiriki siasa.
Mnamo Alhamisi, kiongozi wa chama cha Wiper Stephen Kalonzo Musyoka akiwa Kandara, Muranga, aliwataka viongozi hao wawili kuacha kuzozana. Akizungumza mbele ya Dkt Ruto, Bw Musyoka alisema uhasama wao unagawanya zaidi Wakenya.

Kulingana na Bw Musyoka, vita vya maneno baina yao Dkt Ruto na Bw Odinga vimeanza kurejesha hofu na taharuki nchini, hali ambayo muafaka ililenga kumaliza.

Bw Musyoka alijitolea kupatanisha Bw Odinga na Dkt Ruto akisema malumbano baina yao ni hatari kwa nchi.

“Wakati mwingine nahisi uchungu rohoni nikiwaona Wakenya wakitaka tu kushambuliana. Nimemwambia rafiki yangu Ruto kuwa kulingana na hali ilivyo, nitawaita pamoja na Raila, nikae katikati yao, niwaambie waache (tofauti),” akasema Bw Musyoka.

“Kila wakati malumbano, hata kwa mazishi malumbano, 2022 iko mbali. Wengine wetu tulikuja na roho safi kwa sababu tunapenda nchi hii. Tukubaliane kuwa tuna taifa moja la kujenga, na tudumishe amani,” Bw Musyoka akasema.

Hata hivyo, swali ambalo wengi wanajiuliza ni ikiwa wawili hao watakubali kupatanishwa, haswa ikizingatiwa kuwa tofauti zao zinaendelea kuongezeka kila siku.

Dkt Ruto anahisi Bw Odinga aliharibu uhusiano baina yake na Rais Kenyatta, ambaye walikuwa wameelewana angemuachia uongozi 2022.

Tangu waliposalimiana, Rais amekuwa na uhusiano wa karibu sana na Bw Odinga.

Ruto ashambulia

Ijumaa, licha ya Bw Musyoka kuwashauri kuacha malumbano, Dkt Ruto alizidi kumshambulia Bw Odinga, kuhusu masaibu ya mbunge wa Malindi Aisha Jumwa aliyefukuzwa ODM.

“Wewe ambaye unajifanya bingwa wa kuwatetea wanawake, sasa unaonyesha sura yako halisi kumtimua mwanamke aliyechaguliwa kiti baada ya kuwabwaga wanaume na sasa unamwambia akupigie magoti akuabudu kama msamaha,” Dkt Ruto alisema kupitia akaunti yake ya Twitter.

“Ni makosa gani kujihusisha na Naibu Rais wa serikali ya Kenya, ambayo una ‘muafaka’ nayo. Hila tupu.”