Habari Mseto

Watalii wafurika Lamu kusherehekea Pasaka

April 2nd, 2018 1 min read

NA KALUME KAZUNGU

WATALII wanaendelea kufurika kisiwani Lamu kwa maadhimisho ya sherehe za Pasaka.

Kufikia sasa idara ya utalii ya Lamu tayari imerekodi asilimia 20 zaidi ya idadi ya watalii wanaokodi vyumba kwenye mahoteli tofauti tofauti eneo hilo.

Katika mahojiano na Taifa Leo ofisini mwake, Waziri wa Utalii, Biashara na Viwanda wa Kaunti ya Lamu, Dismas Mwasambu, alisema hoteli mbalimbali za Lamu tayari zimejaa wageni wanaowasili kujumuika na wenyeji katika kuadhimisha Pasaka.

Kamanda wa polisi wa kaunti ya Lamu, Muchangi Kioi. Anasema usalama umeimarishwa kote Lamu msimu huu wa Pasaka ambapo wageni ni wengi. Picha/Kalume Kazungu

Alisema wengi wa watalii wanaozuru eneo hilo kwa sasa ni wale wa ndani kwa ndani.

“Tayari tumerekodi asilimia 20 zaidi ya watalii wanaozuru Lamu msimu huu wa Pasaka ikilinganishwa na wakati wa kawaida. Licha ya kuweko kwa watalii kutoka mataifa ya nje, idadi ya wale wa ndani kwa ndani ambao ni kutoka Nairobi, Mombasa, Kilifi, Watamu na Malindi ni wengi mno,” akasema Bw Mwasambu.

Wakati huo huo, usalama umeimarishwa kote Lamu wakati huu wa sherehe za Pasaka.

Kamanda Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Muchangi Kioi, alisema maafisa wa kutosha wa usalama wamesambazwa kwenye maeneo yote ya Lamu ili kudhibiti usalama msimu huu wa Pasaka.

Baadhi ya watalii waliofika katika kisiwa cha Lamu kwa sherehe za Pasaka. Picha/ Kalume Kazungu

Bw Kioi kadhalika aliwahakikishia wageni na wenyeji ulinzi wa masaa 24 wakati huu wote wa hafla ya Pasaka.

Alisema doria za polisi na jeshi pia zimeongezwa kwenye barabara kuu ya Lamu kuelekea Garsen na akawataka wasafiri kwenye barabara hiyo kuondoa shaka.

“Tuko imara kuhakikisha sherehe za Pasaka zinaadhimishwa kwa amani. Tumesambaza maafisa wetu barabarani, baharini, angani na hata kwenye vijiji vya Kiunga na Ishakani ambavyo viko mpakani mwa Lamu na Somalia,” akasema Bw Kioi.

Aidha aliwataka wakazi na wageni kuwa macho na kuripoti matukio au watu wowote ambao watawashuku kuwa hatari kwa usalama wa taifa.