Habari Mseto

Watalii wafurushwa ufuoni kufuatia hofu ya Kimbunga Hidaya

May 3rd, 2024 2 min read

Na WINNIE ATIENO

MAAFISA wa usalama katika Kaunti ya Mombasa wamepiga marufuku uogoeleaji katika Bahari Hindi kutokana na kimbunga cha Hidaya.

Wakazi na hata watalii wanaopania kujivinjari kwenye fuo za Bahari Hindi wametakiwa kusitisha mipango hiyo.

Hii ni baada ya serikali kutoa tahadhari kuhusu kumbuga hicho kinachotarajiwa kuvuma katika Bahari Hindi, Pwani ya Kenya.

“Bahari imechafuka, kimbuga kilichotangazwa na serikali ni cha kweli ndio maana hii leo niko katika fuo hii kuonya wakazi na watalii kutoogelea. Nimetoa amri kuanzia sasa hakuna mtu anaruhusiwa kuogelea au hata karibu na fuo hii,” alisema Bw Daniel Mumasaba, Kamanda wa Polisi eneo la Nyali.

Alisema kamati ya Usalama ikishirikiana na vyombo vyingine vya usalama wa baharini ikiwemo KMA (Kenya Maritime Authority) inaendelea kushika doria ufuoni.

“Hakuna mtu anaruhusiwa kuingia baharini. Polisi wataendelea kushika doria hadi pale serikali itatangaza kimbunga hicho kimeshapita,” alisisitiza.

Kulingana na Baraza la Mawaziri Nchini, Kimbunga Hidaya kinatarajiwa kuvuma katika Bahari Hindi na kusababisha upepo mkali, mvua na mawimbi makubwa eneo la Pwani.

Kaunti zilizotajwa kuwa na hatari ya kuathiriwa na mafuriko kutokana na utabiri wa hali ya hewa ni pamoja na Kilifi, Taita Taveta, Tana River, Kwale na Lamu. Kaunti hizo za Pwani bado hazijaathirika na mvua kubwa inayoendelea kunyesha sehemu zingine nchini lakini serikali ina wasiwasi kutakuwa na mafuriko.

Tayari Rais William Ruto alishawaonya wakazi wanaoushu nyanda za chini kuhamia nyanda za juu kufuatia mafuriko yanayoendelea kushuhudiwa sehemu kadhaa nchini.

Mafuriko hayo yalisababisha serikali kusitisha ufunguzi wa shule zote nchini hadi Mei 6.

Hata hivyo, mvua inayoendelea kunyesha hasa sehemu za bara na Nairobi inatarajiwa kuathiri ufunguzi wa shule kwa mara ya pili. Hii ni baada ya miundo misingi ya shule kuathiriwa na mvua hiyo hasa madarasa, vyoo, bweni, na uwa.

Wizara ya Elimu iliagizwa kushirikiana na Hazina za Kitaifa za Maendeleo ya Maeneo Bunge (CDF) kukarabati shule hizo.

Baadhi ya magavana wakiongozwa na Fatuma Achani (Kwale), Abdulswamad Nassir (Mombasa) na mwenzao wa Kilifi Bw Gideon Mung’aro wameshatoa tahadhari kwa wakazi wanaoishi katika maeneo yanayoathirika na mafuriko kuhamia maeneo salama wakati huu ambapo ukanda wa Pwani unatarajiwa kushudia mvua nyingi mwezi huu wa Mei.

Huko Kwale, serikali ya kaunti imetaja maeneo yanayoathirika na mafuriko mara kwa mara ikiwemo Vanga, Kiwegu, Majoreni na Jego katika eneo bunge la Lungalunga na Vumbu katika eneobunge la Msambweni.