Kimataifa

Watalii wanene walaumiwa kuvunja viungo vya punda

August 8th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

SANTORINI, UGIRIKI

MALALAMISHI yameibuka kwamba watalii wanene wanafanya punda wa Kisiwa cha Santorini kuwa viwete.

Kisiwa hicho kina umaarufu wa kuvutia watalii ambao hupenda kusafiri kwa punda wanapopanda vilima vidogo.

Lakini sasa watetezi wa haki za wanyama wamejitokeza kulalamika kuwa punda wengi mno wamegeuka viwete kwa kuwa hawana uwezo wa kustahimili uzani wa watalii ambao wengi wao hutoka nchi za Magharibi.

Mashirika ya habari yalimnukuu mwakilishi wa shirika la kutetea haki za wanyama akisema kuwa imebidi shirika hilo kuwachukua punda walioumia ili waanze kutibiwa misuli yao na kufunzwa kutembea vyema.

Mbali na kugeuka viwete, ilisemekana punda wengine huvunjika uti wa mgongo au kuchubuka ngozi.

Kulingana na ripoti za habari, watetezi wa wanyama walisema punda hastahili kubeba uzani unaozidi asilimia 20 ya uzito wake.

Kinyume na hitaji hili, watalii wenye uzani mkubwa walisemekana pia hubeba mizigo ikiwemo hema, vyakula na maji wakielekea juu ya vilima.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba punda hao hufanyishwa kazi kupita kiasi wakati wa msimu wa utalii ambapo huwa kuna joto jingi.

-Imekusanywa na Valentine Obara