Makala

Watalii wang’ang’ania mfupa wa nyangumi kupiga ‘selfie’

February 29th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

KWA waja, mfupa, uwe ni wa wanyama wa kufugwa au wale wa mwituni, huwa ni kitu cha kawaida kuonekana.

Katika mji wa Shela kisiwani Lamu aidha, kuna mfupa wa aina yake ambao miaka ya hivi karibuni umegeuka kuwa kivutio cha watalii na wageni.

Kila anayetembelea mji wa Shela, iwe ni mtalii au mgeni wa ndani kwa ndani au yule wa kimataifa, huishia kumiminika mahali ulipo mfupa huo huku waking’ang’ania kujipiga picha wenyewe kwa upande wa mbele wa kamera ya simu, almaarufu ‘selfie.’

Je huu ni mfupa gani na ni nini hasa upekee wake?

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa kinachong’ang’aniwa na watalii na wageni hao ili kupata fursa ya kupiga picha nacho kwenye mji huo wa Shela si mfupa tu bali ni kiunzi cha mifupa ya nyangumi.

Kwa wale wasiofahamu, nyangumi ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye umbo kama la samaki.

Nyangumi yuko katika jamii ya mamalia ambao ni wanyama wenye kuzaa viumbe na kunyonyesha.

Aghalabu nyangumi huwindwa baharini kwa sababu ana mafuta mengi sana.

Kulingana na wanajamii wa Shela, hasa wazee, kiunzi hicho cha mifupa ya nyangumi kilisafirishwa zamani na wavuvi waliopata mzoga wa mnyama huyo ndani ya bahari ya kina kirefu akiwa amekufa na kuoza yapata zaidi ya miaka kumi iliyopita.

Mzee wa Shela, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wahudumu wa Matembezi ya Watalii Ufuoni kaunti ya Lamu, Bob Abdalla, anakiri kuwa sio rahisi kumpata nyangumi, awe hai au akiwa tayari amekufa.

“Ilikuwa tu bahati wavuvi wetu walipopata mzoga wa nyangumi ndani ya Bahari Hindi eneo hili la Shela. Walishirikiana kuubeba mzoga hadi ufuoni ambapo uliachwa kuoza na kukauka kabisa hadi kikabakia kiunzi hicho cha mifupa. Hapo ndipo jamii kwa ushirikiano na mshikadau kutoka ng’ambo wakaafikia kutengea kiunzi hicho cha mifupa ya nyangumi mahali maalum ambapo kimehifadhiwa na kuwa kama maonyesho kwa wanaofika Shela,” akasema Bw Abdalla.

Ikumbukwe kuwa mbali na Mji wa Kale wa Lamu, Shela pia ni miongoni mwa maeneo yanayotambuliwa kuwa ngome kuu za watalii wanaozuru Kenya, hasa, kaunti ya Lamu.

Kiunzi cha mifupa ya nyangumi kilichoko eneo la Shela, Lamu. Mifupa hiyo ya nyangumi imekuwa iking’ang’aniwa na watalii kupiga ‘selfie’. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Abdalla anafichua kuwa kuwepo kwa kiunzi hicho cha mifupa ya nyangumi eneo lao la Shela kumeleta manufaa tele kwani wengi wamekuwa wakisafiri mbali na karibu kufika eneo hilo kujionea taswira kamili ya mifupa ya nyangumi inayoonekana kuwa sawa na ‘maajabu ya ulimwengu.’

“Kila mtalii anayefika hapa Shela si rahisi kuondoka baada ya likizo yake bila kufika eneo kulikowekwa kiunzi cha mifupa ya nyangumi angalau kupiga picha pale na kugusagusa mifupa hiyo. Yaani kwa wengi haya ni maajabu ya ulimwengu. Twafurahia jinsi kiunzi hicho cha mifupa ya nyangumi kimegeuka kuwa kivutio cha watalii na wageni,” akasema Bw Abdalla.

Kwa upande wake, mzee mwingine wa Shela, Bw Khuzema Mohamed Salim, anasema mbali na kuwa kivutio cha watalii, kiunzi cha mifupa ya nyangumi kilichoko Shela pia kihistoria kimegeuka kuwa kitambulisho au dhihirisho kamili kwamba Shela ni eneo la uvuvi.

Kadhalika, kuwepo kwa kiunzi hicho cha mifupa ya nyangumi pia ni idhibati kamili kwamba kwenye Bahari Hindi eneo la Shela na Lamu hupatikana viumbe wakubwa wa baharini kinyume na maeneo mengine ya nchi na ulimwengu.

“Twajivunia kwamba hii mifupa ya nyangumi iliyoko hapa Shela imeuza sera za Lamu kuwa eneo lenye utajiri mwingi wa viumbe wakubwa baharini. Pia inaleta taswira kamili kwamba kihistoria mji wetu wa Shela na Lamu kwa ujumla ni maeneo mahiri kwa uvuvi,” akasema Bw Salim.

Baadhi ya watalii wa ndani kwa ndani na wale wa kimataifa waliohojiwa na Taifa Leo hawakuficha furaha yao kwa kufika Shela kila mara kujionea kiunzi hicho cha mifupa ya nyangumi.

Kiunzi cha mifupa ya nyangumi kilichoko eneo la Shela, Lamu. Mifupa hiyo ya nyangumi imekuwa iking’ang’aniwa na watalii kupiga ‘selfie’. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bi Beatrice Atieno, mtalii kutoka Kisumu, anasema yeye binafsi hajaona nyangumi akiwa hai ila tu wale wa pichani au runingani.

Bi Atieno anasema alianza kuhisi mvuto wa kufika Lamu pale aliposikia kwamba kuna sehemu ambapo kiunzi cha mifupa ya nyangumi kimehifadhiwa.

“Kila mwaka nikija Lamu lazima nifike hapa Shela kupiga picha na hii mifupa ya nyangumi. Kweli ni mnyama mkubwa wa baharini. Nimemuona nyangumi akiwa hai kwenye filamu za uhifadhi wa mazingira na viumbe hai baharini runingani pekee na wala si ana kwa ana,” akasema Bi Atieno.

Edward Archie, mtalii kutoka Uingereza, alisema yeye amemuona nyangumi akiwa hai baharini lakini alikuwa hajaona mifupa au kiunzi cha mifupa ya mnyama huyo.

“Hii ndiyo sababu baada ya kutembelea eneo hili la Shela na kujulishwa kuwa hiki ni kiunzi cha mifupa ya nyangumi, sikusita kupiga picha hapa ili ziwe kumbukumbu nitakayoonyesha familia yangu punde nikirudi Uingereza hivi karibuni,” akasema Bw Archie.

Sehemu mojawapo ya kisiwa cha Shela. Ni miongoni mwa maeneo ya Lamu ambayo huvutia watalii. PICHA | KALUME KAZUNGU