Watambue wanawake bomba walio chini ya miaka 30

Watambue wanawake bomba walio chini ya miaka 30

LILYS NJERU NA WANGU KANURI

Kwa Muhtasari

Mnamo Januari, tuliuliza maoni ya watu katika sekta mbalimbali, ili kuunda orodha ya wanawake wapevu wenye umri wa miaka chini ya 30 ambao wanafanya bora katika nyanja zao. Hata ingawa kila mtu aliyetajwa alistahili kuangaziwa, tulihitaji kupunguza orodha hii. Ikatulazimu tuwe na wanajopo ambao wangetathmini orodha ile na kutupatia majina ya wale waliofuzu.

Waliwachagua kina nani hasa?

Mwaka jana, baada ya janga la corona kustakimu nchini Kenya, miezi iliyofuatia wananchi wengi walikumbwa na hali ya sintofahamu. Hali kadhalika, wiki hii chanjo zilitua nchini lakini bila pingamizi yoyote, ugonjwa wa corona ulibadilisha maisha yetu kabisa.

Ni dhahiri kuwa tunapoendelea na mwaka wa 2021, watu wenye azma ya mabadiliko wanahitajika sana. Tunapoadhimisha siku ya wanawake ulimwenguni, jarida la Jumamosi lilitaka kuwajua ni wanawake wapi wapevu wanashikilia siku za usoni kwani vijana ndio imani ya kesho.

Tunawaletea wanawake bomba ambao wapo chini ya miaka 30 na ambao wanayaboresha maisha yao na kuziunda misingi ya mabadiliko ambayo itawahamasisha watu kichanya sio tu kwa mwaka wa 2021 bali kwa miaka ijayo.

Dkt Gladys Chepkirui Ngetich, 29, mhandisi wa anga

Kutoka kujiunga na shule ya msingi ya Lelaibei katika kaunti ya Nakuru hadi chuo kikuu cha Oxford nchini Uingereza, safari ya kiakademia ya Chepkirui inatia mtu moyo sana. Wakati Chepkirui alijizolea alama 298 kwa 500 katika mtihani wake wa kitaifa KCPE mwaka wa 2004, watu walidhani kuwa hataenda mbali kimasomo.

Miaka minne baadaye, aliibuka mwanafunzi bora katika wilaya ya Kipkelion huku akijizolea gredi ya A- ambayo ilimsaidia kupata udhamini wa James Finlay. Katika chuo kikuu cha JKUAT, Chepkirui alisomea uhandisi wa mitambo na kuwa mmoja kati ya wasichana 9 waliokuwa wakisomea taaluma hiyo katika jumla ya wanafunzi 80. Chepkirui alifuzu na digrii ya daraja la kwanza mnamo 2015 na akapata udhamini mwingine kule UK.

Hivi sasa, Chepkirui anaufanya utafiti wake wa digrii ya uzamifu katika kundi la utafiti la Space Enabled chini ya ushirika wa kisayansi wa Schmidt. Chepkirui alifuzu uzamifu wake katika chuo cha Oriel akiwa na miaka 28.

Zaidi ya masomo yake yenye kufana kwingi, Chepkirui huwapa motisha watu, yeye ni mwanariadha na mwanasoka na anahamu nyingi katika kumkuza mwanamke. Isitoshe, yeye ni mmoja wa waziunduzi wa Iluu, shirika la kujikuza la kijamii na ameshirikiana katika uandishi wa kitabu The Bold Dream: Transcending the Impossible. Kitabu hiki kimenuia kuwapa moyo vijana kwani kimenakili safari yake ya elimu kinagaubaga.

Betty Kingori, 27, Mwanzilishi wa TEDxParklands.

Mnamo 2017, Betty aliongoza darasa lake kwa digrii ya daraja la kwanza huko JKUAT. Mwaka uo huo, alishinda tuzo la nafasi ya kwanza kwa uvumbuzi wa toleo la nane la JKUAT TECH EXPO 8.0 liliokuwa “The Fabrication of a Domestic Avocado Oil Extractor.”  Baadaye, alichaguliwa kushiriki katika kikundi cha ushirikiano wa viongozi wavumbuzi ambacho kilikuwa ushirikiano kati ya serikali ya Kenya na Uingereza. Alipokea mafunzo kutoka London na kupokea ruzuku ya kuuza mafuta ya parachichi yaliyotokana na uvumbuzi wake.

Mnamo 2019 Betty alijiunga na chuo kikuu cha Edinburgh alipofanya digrii yake ya uzamili. Mwaka huu Betty analenga kufanya digrii yake ya uzamifu katika uhandisi wa mitambo akilenga vifaa vya uhandisi, utengenezaji na uzalishaji. Anapania kuboresha uvumbuzi wake ili kuyaimarisha maisha ya wakulima wa parachichi nchini Kenya na barani Afrika.

Hapo awali Betty, alifanya kazi na KPMG na alikuwa mfanyabiashara katika kampuni ya kwanza kutengeneza viatu vya kitaalamu vya kukimbia. Yeye pia ni mwenye leseni na kiongozi katika TEDxParklands. Betty alikua katika eneo la Maziwa kaunti ya Nairobi ambapo baada ya kuhitimu masomo yake ya kidato cha nne mnamo mwaka wa 2011, alipokea udhamini wa serikali wa kusomea digrii yake ya uhandisi wa mitambo katika chuo kikuu cha JKUAT.

Sarafina Mumbi, 25, msanii wa graffiti

Anapokuwa shuleni, Mumbi anafahamika kama Tsara Arts. Mumbi alipendezwa sana na rangi nzuri za matatu ambazo zilikuwa zikiwabeba abiria wa Mathare pale ambapo alilelewa.

Hata hivyo, alielewa fika kuwa kuingia katika sekta ya matatu ambako ni nyanja ya wanaume itakuwa na ugumu wake. Mnamo 2014, mmoja wa rafiki zake alikubali kumfunza kila kitu kuhusiana na uchoraji wa magari. Kutoka hapo, amezirembesha matatu zisizo na idadi. Hata ingawa amekumbana na changamoto kama kudunishwa kwa kuwa mwanamke katika nyanja hii, bado hajaibadilisha nia yake na anawatia moyo wanawake wengine kumuunga katika nyanja hii.

Elizabeth Wathuti, 25, mwanamazingira 

Elizabeth anayejulikana sana kama Liz Maingira ni mvumbuzi wa Green Generation Initiative na mshindi wa uandishi wa blogu za mazingira. Akiwa mwenye umri wa miaka 17, Elizabeth alipanda mti wake wa kwanza Karima Hill iliyoko kaunti ya Nyeri, nyumbani kwao kisha akaenda kuifufua klabu ya mazingira katika shule ya upili ya Kangubiri. Alipokuwa katika chuo kikuu cha Kenyatta ambako aliifanya digrii yake katika masomo ya mazingira na ukuzi wa jamii, aliongoza katika klabu ya mazingira katika chuo hicho (KUNEC) kwa miaka mitatu mtawalia.

Ameongoza hafla nyingi za upanzi wa miti ambazo zinajumuisha kutembelea shule na kuzungumza na wanafunzi. Hamasisho lake kuu hutoka kwa marehemu Wangari Maathai ambaye alitoka Tetu. Cha kushangaza ni kwamba alikuwa mpokezi wa nne wa udhamini wa Wangari Maathai kupitia Greenbelt Movement. Elizabeth ana maono ya dunia ambayo watu wataishi kwa amani na mazingira yao na dunia ambayo watu watachunga mazingira yao.

Passy Amayo Ogolla, 28,  mwanaharakati wa mazingira Afrika

Passy Amayo ni kiongozi anayejitolea na anahamu ya kuwakuza vijana, kurejesha urembo wa mazingira na hatua za tabianchi na siku za usoni za nishati endelevu nchini Afrika. Ameonyesha hamu na kujitolea kwingi katika kazi yake kama meneja wa programu katika Society for International Development (SID)

Passy amejihusisha na United Nations Major Group for Children and Youth (UNMGCCY) ambapo anahudumu kama Regional Focal Point for Eastand South Africa katika wadi ya vijana ya SDG 7. Anafanya kazi na wanamazingira katika upanzi wa misitu ya matunda kule alikozaliwa. Hivi majuzi, Passy aliteuliwa kama Africa Network Weaver for the Next Generation Foresight Practice chini ya shule iliyomo London ya International Futures. Zaidi ya kuandika kuhusu tabianchi, anahamasisha tabia na mabadiliko ya sera katika siku endelevu za usoni.

Nikita Kering, 19, Mwimbaji/ mtunzi wa nyimbo

Nikita ni mmojawapo wa wanamuziki wapevu sana ambao wanazidi kutingisa sekta ya burudani. Alivuma akiwa mwenye umri wa miaka 16 baada ya wimbo wake Tragedy kupasua miamba ya usanii. Wimbo huu ambao huzungumzia hisia halisi za mahabubu unaeleza kwa kina vurugu kati ya wapendanao.

Mnamo 2017, Nikita alijizolea tuzo mblili ambazo ni Best Eastern Africa Female Artiste of the Year na Revelation of the African Continent. Tuzo hizi zilimfanya kuingia katika kumbukumbu za kihistoria kama mshindi mpevu katika tuzo la Africa Music mwaka wa 2019. Tangu alipotoa wimbo wake wa kwanza, nyimbo zake zimepokea tuzo nyingi na kupendwa sana.

Nadia Mukami 24, mwanamuziki na mtunzi wa nyimbo

Nadia Mukami Mwendo ni mmoja wa wanamuziki bora wa kike sio tu nchini Kenya lakini barani pia. Nadia alianza kusomea uimbaji mwaka wa 2015 baada ya kuutoa wimbo wa Barua Ya Siri akiwa bado mwanafunzi katika chuo kikuu cha Maseno. Hata hivyo ni wimbo wake Kesi ambao ulimfahamisha kwa dunia na akapata kushirikiana na nyota wa muziki katika tamasha kama zile za Blaze na Safaricom, Nile na tamasha la Luo.

Mwaka huu aliteuliwa kwa mara ya kwanza katika tuzo la MTV Afrika la Muziki (MAMA) akimenyana na wasanii kama Diamond Platnumz, Wizkid na Fally Ipupa. Mnamo 2019, wimbo wake Radio Love ulijizolea tuzo mbili katika tuzo za Pulse Music (PMVA). Isitoshe mwaka wa 2020, Nadia alitanganza kuwa ametengeneza milioni yake ya kwanza na akatoa EP ambayo inakaribia milioni 10 ya kuonekana. Kauli inayomwongoza ni “Jitihada hulipa.”

Neema Nkatha, 26, nguo za kuogelea Ohana

Neema ni mwanzilishi wa Ohana Family Wear Limited na nguo za kuogelea za Ohana . Alianzisha biashara hizi baada ya kugundua kuwa nguo za kuogelea za Kiafrika zilikuwa ngumu kupata. Alifanya kazi na marafiki zake na watu waliobebea katika kubuni mitindo na akaunda mitindo yake na kukuza biashara kutokana na mitindo hiyo.

Hivi sasa nguo za kuogelea za Ohana zimevaliwa katika wiki ya fasheni ya London na ameuza nguo za kuogelea 2000. Neema ni mmoja wa watu walio katika programu ya Creative DNA ambayo hunuia kusaidia biashara za fasheni nchini Kenya.

Ann Wanjuhi Njoroge, 20, Mwanzilishi wa Nelig Group

Wanjuhi anapenda sana watu na sayari na amepata uzoefu mwingi katika kufanya kazi na jamii za kijijini haswa wale wanaoishi katika misitu pamoja na kusaidia ajenti na mashirika ya kiserikali katika kujumuisha maendeleo katika biashara zao.

Wanjuhi amehitimu masomo yake ya chuo kikuu huko katika chuo kikuu cha Nairobi ambapo alisoma taaluma mbili ya Soshologia na Mawasiliano. Isitoshe yeye pamoja na Eva Njoki wamezianzia kampuni mbili The Web Tekies ambayo huwasaida watu na mabiashara ya kupatiana hadithi zao kupitia vyombo vya habari na RootEd Africa ambayo alianzia kwa sababu ya kupenda mawasiliano kwa vyombo vya habari.

Wanjuhi pia ni mwanzilishi wa Nelig group. Pia yeye ni mmoja wa Vital Voices na memba mdogo katika kamati ya kaunti ya Nyeri ya Affirmative Action Social Development Fund (AASDF). Isitoshe yeye pia ni mmoja wa timu inayotekeleza intaneti kwa All Project by the World Economic Forum inayolenga kuwaunganisha watu milioni 25. Pia alipokea tuzo la top 40 under 40 mwaka wa 2016.

Sharon Wendo, 29, Mwanzilishi wa vito vya Epica

Kutoka kuwa mpokezi wa watu, Sharon alisoma jinsi ya kutengeneza vito kupitia mitandao ya kijamii. Miezi michache kabla, Sharon alitoa mkusanyiko wake wa kwanza na wiki mbili zilizopita, vito vyake vilitumika katika fasheni ya wiki ya London. Vito vyake vimeonyeshwa katika chapisho la Harper’s Bazaar Italia na Vogue Italia.

Sharon hupata ubunifu wake kutoka kwa utamaduni wa Afrika na fasheni ya kisasa na ananuia kuziunganisha ulimwengu hizi mbili katika utengenezaji wa vito vyake.

Katika mahojiano ya hivi karibuni, Sharon alisema kuwa anataka kuwafunza watu ujuzi ufaao ili mtu aanzie biashara yake na awatafute washirika wa kimataifa.

Brigid Kosgei, 27, mwanaspoti

Alipokuwa akienda shuleni, Brigid alipatana na wanariadha wakifanya mazoezi na akatamani sana kuwa kama wao. Alilelewa na ndugu zake 6 na mamake katika kaunti ya Elgeyo Marakwet, kaunti inayovuma sana kwa kuwatoa wanariadha bora nchini. Alipogundua kuwa mamake alikuwa anataabika kulipa karo ya shule, aliacha shule na akaanza kukimbia. Baada ya miezi, alikimbia katika mbio za masafa marefu za kwanza Novemba 2015 kule Portugal na kuja nambari moja. Brigid amejishindia tuzo nyingi. Alishinda mbio za masafa marefu za 2018 na 2019 za Chicago na mbio za masafa marefu za 2020 za London. Hivi majuzi aliteuliwa kwa tuzo la dunia la mwanaspoti mwanamke wa mwaka wa 2020.

Mwezi jana, Brigid alithibitishwa katika timu ya mbio za Kenya ambazo ziliahirishwa hadi 2020 Olimpiki za Summer.

Faith Ogalo, 27, mtaalamu wa Taekwondo

Faith ndiye mkenya pekee aliyefuzu katika shindano la taekwondo ambalo lilikuwa lifanyike Tokyo lakini sasa limeahirishwa. Mnamo 2018, Faith alikuwa akicheza mpira wa kikapu katika chuo kikuu cha Kibabii ambako alikuwa akifanya digrii yake katika kazi ya jamii. Kochi mmoja alimtambua na kumshawishi ajiunge na Taekwondo. Azimio lake lilimfanya kuteuliwa katika timu ya chuo hicho kikuu ambacho hushiriki katika michezo ya mwaka ya vyuo vikuu nchini Kenya.

Toka hapo, Faith amekuwa akishindana katika mashindano kadha wa kadha kama Mombasa Chairman’s Cup, Korean Ambassador Cup, Tanzania Korean Cup na Rwanda Genocide Memorial Tournament huku akiwa katika timu ya chuo hicho cha Kibabii. Isitoshe amekuwa akifuzu kwa zote.  Baada ya kufuzu vizuri, Faith alipokea mwaliko wa kujiunga na timu ya Kenya ambapo anajiandaa kuwakilisha Kenya katika jukwaa wakati siku nyingine itatangazwa ya michezo ya Olimpiki nchini Tokyo.

Ashura Michael, 27, Mtetezi wa haki za binadamu na jinsia

Ashura ni mwanamke mpevu ambaye anawakilisha uvumilivu na kujitolea kwingi. Alipokuwa mwenye umri wa miaka minne, alipoteza uwezo wa kusikia kwa sababu ya ugonjwa wa surua. Hata hivyo, jambo hilo halikumzuia kuhudumu katika nafasi za uongozi na nyanja zingine za jamii. Anaongoza kama mmoja wa wakurugenzi katika bodi ya kiserikali ya watu wanaoishi na ulemavu na mwenyekiti msaidizi wa Kenya Chapter of the Africa Charter kwa Demokrasia, Uchaguzi na Uongozi. Ashura ni kiziwi wa kwanza kuchaguliwa kama spika wa mkutano wa EALA Vijana. Pia alihudumu kama katibu mkuu katika kitengo cha vijana katika Kenya National Association of the Deaf.

Ashura amehitimu digrii yake katika ujinsia na maendeleo katika chuo kikuu cha Nairobi na hivi sasa anasomea sheria katika chuo hicho. Anahamu nyingi ya kuzitetea haki za watu wanaoishi na ulemavu na ananuia kufanya hivyo kupitia masomo ya uongozi, sheria na maendeleo.

Banice Mbuki Mburu, 27, Mtetezi wa uundaji wa sera za umma

Banice anatajiriba ya miaka zaidi ya tano katika uundaji wa mikakati ya maendeleo, sera za umma, uchambuzi na haki za kijamii. Yeye ni mshindi wa Top 35 under 35 Change Makers barani Afika chini ya kitengo cha Advocacy and Community Action. Nchini Kenya ameshirikiana katika uzinduzi wa miradi ya vijana, akajihusisha na kamati za kiufundi ambazo ziliohoza na vitengo mbalimbali kwa madhumuni ya kuzikuza na kuzidurusu sera zinazowadhuru watu wapevu na kutetea Public Interest Litigation ili ziwasaidie vijana.

Banice ni mmoja wa vijana 15 ambao walichaguliwa Afrika ili kuongoza katika kutamatika kwa Model African Union Toolkit ili kuwawezesha vijana kujiunga na Umoja wa Afrika. Sababu ya kazi yake kuhusu ngono na haki za afya ya uzazi nchini Kenya na Afrika Kusini, rais wa United Nations General Assembly alimteua azungumze katika United Nations General Assembly (UNGA) wakati wa kukumbuka International Conference on Population and Development (ICPD @25)

Banice anapiga hatua katika kazi yake kupitia kampeni ya Sauti Sasa, kampeni inayonuia kuzungumzia kuhusu mimba za wanarika nchini Kenya. Yeye ni mratibu wa kitaifa na wa kaunti wa kampeni za afya za AMREF Afrika, memba wa bodi ya Siasa Place, mkusanyaji wa muungano wa shirika la Youth Serving na mratibu wa Youth for Tax Justice Network nchini Kenya.

Nadia Ahmed 29, Waziri Msaidizi katika Wizara ya ICT

Mapema mwaka jana Nadia aliteuliwa CAS. Kabla kuteuliwa kwake, Nadia alizaliwa na kulelewa katika Marikiti, Mombasa aliongoza hafla za vijana na wanawake kuhusu afya ya akili na akagundua kuwa kuna uhusiano kati ya wanawake wanaopitia vurugu za kinyumbani na wanasaikolojia baada ya kuhitimu digrii yake ya uzamili nchini Berlin.

Katika jukumu lake mpya, Nadia ananuia kusaidia kujenga mazingira mazuri ambayo yanaipa kipaumbele maendeleo, ushirikiano na upanuzi wa matumizi wa teknolojia ya habari na mawasiliano akiwazisaidia miradi za uvumbuzi za vijana. Nadia pia ni mwenyekiti msaidizi katika bodi ya UNDP Kenya Youth Sounding ambayo ni ushirikiano wa mashauriano kati ya UNDP na wizara ya ICT ambayo hukakikisha kuwa vijana wamejumuishwa katika uamuzi.

Jihan Abass, 26, Mwanzilishi bima za Lami

Jihan alizindua kampuni ya bima ya kwanza nchini Kenya ya kidijitali ya magari pekee ambayo humwezesha mteja kulipa kwa awamu na kusimamisha malipo haya iwapo mteja huyu atasafiri nje ya nchi. Griffin Motor App ni moja wa bidhaa za Lami na imefupisha harakati za ununuzi wa bima ya gari kwa muda wa chini ya dakika mbili. Kabla ya haya, Jihan alifanya kazi kama muuzaji wa sukari kule London huku akiuza katika soko za sukari za New York na London. Ana digrii yake katika uzamili katika chuo kikuu cha Oxford na digrii yake kutoka chuo cha kibiashara cha CASS, London. Mwaka uliopita, Jihan alichaguliwa kuwakilisha Afrika katika World InsureTech Connect (ITC) 2020.

Dorcas Owinoh 29, Mwanzilishi mwenza wa LakeHub

Dorcas alizaliwa na kulelewa Kibera ambako alishindwa kupatana na teknolojia. Hivi sasa Dorcas anafanya kazi na wasichana kutoka maeneo kama yale aliyotoka na kuwasaidia kupata teknolojia. Mwaka wa 2018, Dorcas alishirikiana katika kuanzisha LakeHub, kitovu cha teknolojia na uzinduzi wa kijamii katika kaunti ya Kisumu ambacho huwasaidia wanajamii wabunifu, waanzilishi wa program, wanaounda mitindo na waanzilishi wa biashara huku wengi wakiwa wasichana wenye umri kati ya miaka 13 na 19. Moja kati ya uvumbuzi wake Dorcas ambao umefanikiwa ni iCut ambayo ni app inayowaunganisha wasichana walioathiriwa na ukeketaji. Wasichana hawa husaidiwa kisheria na kimatibabu. Dorcas alitambuliwa na Forbes Africa 30 under 30 na akawa mshindi wa pili katika tuzo la Queens Young Leaders, 2018.

Elsa Majimbo, 19, Mcheshi

Katikati ya kipindi cha janga la Corona, wengi walitambulishwa kwake Elsa Majimbo, mcheshi wa Instagramu ambaye aliunda mazungumzo ya nafsi yake na kutamatisha kwa kicheko huku akivalia miwani yake na akila vibanzi. Hata ingawa alianza kubuni mazungumzo haya ya kinafsi mwaka wa 2016, alivuma mwaka wa 2020 wakati ambapo mwigizaji Lupita Nyong’o alisambaza video yake moja. Chini ya mwaka mmoja, nyota huyu anazidi kung’aa huku akiwa na wafuasi zaidi ya milioni 2 Instagramu.

Mchezaji huyu bomba wa awali wa chesi na mwanafunzi wa taaluma ya Mawasiliano katika chuo kikuu cha Nairobi, sasa ni balozi wa Fenty beauty (brandi ya mapambo ya Rihanna), akishirikiana pia na MAC. Elsa ameteuliwa kwa tuzo la Nickelodeon Kids Choice na akashinda tuzo la E! People’s Choice katika kikundi cha African Social Star. Hivi majuzi alitia saini mkataba na kampuni ya mitindo ya Kiitaliano, Valentino.

Majimbo alionyeshwa katika kipindi cha Netflix cha Strong Black Lead pale ambapo alizungumzia changamoto za kutopata fursa sababu ya rangi yake nyeusi. Majimbo anasema kuwa anashawishiwa na nafasi yake ya ubaguzi wa rangi na jitihada yake katika kumfanya kila mtu ajihisi starehe kwa ngozi yake.

Foi Wambui, 23, Mwigizaji

Foi Wambui ni mtangazaji wa redio na televisheni na mwenye kupewa tuzo la uigizaji na uandishi wa maigizo. Foi alianza kuigiza akiwa shule ya sekondari na hata kujizolea tuzo la mwigizaji bora katika tamasha za drama mwaka wa 2014. Mwanafunzi huyu wa taaluma ya mawasiliano katika chuo kikuu cha USIU ameigiza majukumu mbalimbali. Mnamo 2020, aliigiza kama rafiki mcheshi wa Nick Mutuma katika filamu ya Sincerely Daisy. Uigizaji huo ulimfanya kujizolea tuzo la Kalasha la muigizaji wa kike bora. Hivi sasa  yeye ni nyota katika filamu ya utani ya Maisha Magic ya Anda Kava akiwa na Njugush na Abel Mutua. Pia yeye ni anaongoza katika kipindi cha Crime na Justice kinachoonyeshwa Showmax.

Dkt Njoki Chege, 30, Mkurugenzi, Kituo cha Ununifu, Chuo Kikuu cha Aga Khan

Katika chuo kikuu cha Aga Khan, Njoki ni kielelezo cha kuunga mkono kizazi kijacho cha wakurugenzi wa vyombo vya habari na viongozi kupitia mafunzo, ushauri na misaada ya wavumbuzi kutoka Kenya, Tanzania na Uganda. Njoki amehitimu digrii yake ya uzamifu katika taaluma ya mawasiliano na masomo ya vyombo vya habari. Isitoshe ana tajiriba ya miaka zaidi ya 9 katika vyombo vya habari kama mwanahabari na edita. Nyuma kidogo amefunza kozi za digrii katika chuo kikuu cha Daystar.

Celestine Olilo, 30, Mhariri wa jarida la MyNetwork na mwanahabari wa spoti

Celestine ni mwanahabari wa spoti aliyejizolea tuzo la mwaka, nafasi iliyotuzwa kwenye Tuzo za Mwaka za Baraza la Uanahabari Kenya (AJEA).

Mnamo 2018, alikuwa miongoni mwa waliochaguliwa kwa tuzo la AIPS kwa hadithi bora ya rangi na kama mtafiti wa spoti wa kike, alichapisha karatasi tatu kuhusu kutumia vyombo vya habari katika kugundua usawa wa jinsia katika spoti.

Katika uchapisho wa My Network, anaangaza hadithi ambazo huwahamasisha vijana katika ukuzaji wa kazi zao. Hivi sasa yeye ni mwanafunzi wa digrii ya uzamifu katika chuo kikuu cha Nairobi.

You can share this post!

Auka Gecheo ataka Kenya kufanya zaidi kufikia Uganda kwenye...

Shirika la The Voice Kiambu lafadhili watoto mayatima