Habari Mseto

Watano wafa kwenye mafuriko

October 24th, 2019 1 min read

Na MANASE OTSIALO na SAMMY LUTTA

WATU watano wakiwemo watoto ni miongoni mwa watu waliouawa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua inayonyesha kote nchini.

Watoto wanne walifariki eneo la Eldas katika Kaunti ya Wajir na mtu mmoja akasombwa katika Kaunti ya Turkana.

Kamishna wa Kaunti ya Wajir, Loyford Kibaara alisema watoto hao walisombwa na mafuriko walipokuwa wakicheza.

Bw Kibaara alisema maeneo ya Bute na Buna ndiyo yameadhirika zaidi na wakazi wamelazimika kuhamia maeneo ya miinuko.

Katika kaunti ya Turkana, mwanamke alisombwa na maji Jumanne jioni kijijini Lorugum.

Mshirikishi wa Shirika la Msalaba Mwekundu katika kaunti hiyo, Bw Nick Thuo alisema mvua iliyopitiliza kiwango iliyoendelea kunyesha Jumatano ikiandamana na upepo mkali iling’oa mapaa ya nyumba kadhaa mjini Lodwar na kuangusha miti.

Mvua iliyopitiliza kiwango pia iliendelea kunyesha maeneo mengine ya nchi.