HabariSiasa

Watapeli kwa jina la Rais

October 3rd, 2019 2 min read

Na DAVID MWERE

AFISI ya Rais imelalamika vikali kwamba wanasiasa, wafanyibiashara, makatibu wa wizara na maafisa wengine wa umma wamekuwa wakitumia jina la Rais Uhuru Kenyatta kwa njia isiyofaa, ikiwemo kutapeli watu.

Matapeli hao, hutumia jina la Rais kujipatia umaarufu serikalini, ikiwemo kukiuka sheria za ununuzi ili kuendeleza maslahi yao ya kibinafsi. Wanapokabiliwa na shutuma za ukiukaji wa sheria hizo, maafisa hao wakiwemo viongozi wa taasisi za umma, wamekuwa wakidai kwamba hulazimika kutoa zabuni moja kwa moja kutokana na maagizo kutoka kwa afisi ya rais.

Lakini Msimamizi wa Ikulu, Bw Kinuthia Mbugua, jana alieleza Kamati ya Bunge inayofuatilia matumizi ya Pesa za Umma (PAC) kwamba, watu kama hao wanapaswa kubeba misalaba yao.

“Sote tunawajibika kuhusiana na masuala yoyote yanayohusu raslimali za umma. Niko katika Ikulu lakini huwa sitaji jina la rais ninapokabiliwa na matatizo. Siwezi kuja hapa na kusema niliagizwa na rais kufanya hili au lile,” alisema Bw Mbugua.

Alifichua kuwa, watu hao mara kwa mara hutafuta kandarasi au kutaka wafanyiwe fadhila zinazowanufaisha kama watu binafsi, wakidai kwamba wametumwa na Rais.

Bw Mbugua aliitaka kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Ugunja, Bw Opiyo Wandayi, ielimishe maafisa wa umma na wafanyibiashara kwamba Rais hawezi kumtuma mtu bila ya nyaraka rasmi au yeye mwenyewe kuzungumza.

Alitoa mfano wa sakata ya mashindano ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 18 ya Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) mnamo 2017, ambapo karibu Sh1.7 bilioni huenda zilipotea kutokana na shughuli za ununuzi za kutiliwa shaka.

Mashindano hayo yaliyofanyika Kasarani, Nairobi kuanzia Julai12- 16, yalishuhudia watu mbalimbali waliohusika katika ununuzi wa bidhaa wakidai kwamba waliagizwa na rais kutumia njia ya ununuzi wa moja kwa moja kwa sababu hakukuwa na muda wa kutumia njia ya utowaji zabuni.

Afisi ya Mkaguzi Mkuu ilifichua ubadhirifu huo katika ripoti yake ya ukaguzi wa rekodi za kifedha mnamo Julai 10, 2018.

Matapeli wamekuwa wakipiga simu au kujiwasilisha na kutaka wapewe kandarasi au nafasi za ajira wakitaja jina la rais bila ya kuwa na nakala zilizoandikwa kutoka kwake, jambo ambalo Bw Mbugua anasema ni kinyume na sheria.

“Katika hali yoyote ile, maamuzi ya rais ni sharti yawe katika maandishi. Yafaa yawe yametiwa sahihi na rais na yanafaa kuwa na muhuri wa kitaifa kwa mujibu wa Kifungu cha 135 cha Katiba,” akasema Bw Mbugua.

Hivyo basi, alionya kwamba kutajwa kwa jina la rais na maafisa wa serikali ili kujitoa mashakani ni jambo lisilofaa.

“Maafisa wote wa uhasibu serikalini kila mara wameagizwa kutotii wito wowote unaodai kutoka kwa rais,” alisema Bw Mbugua, ambaye pia ni msimamizi wa matumizi ya fedha katika afisi ya rais mbele ya kamati iliyoongozwa na Bw Wandayi.

Bw Mbugua alieleza kamati kwamba, rais hujitahidi kuhakikisha maafisa wanaofaa wamo afisini na wako tayari kutekeleza na kuendeleza sera za serikal,i pamoja na kuwa tayari kuwajibika.

“Ndio maana bunge huchangia pakubwa kupitia upigaji msasa kuhakikisha tuna watu wanaofaa katika huduma za umma. Hivyo basi wanapogeuka na kutaja jina la rais, ni ishara kuwa hawana ukakamavu au hawafahamu chochote kuhusu wanachohitajika kufanya,” akasema.

“Maafisa mbalimbali wa taasisi za umma huja hapa wakidai walipatiwa maagizo mahsusi kutoka ikulu kuhusiana na shughuli za ununuzi. Mbona iwe hivyo,” alihoji Mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro.