Habari Mseto

Watatu wachomwa kwa kuiba kuku kijijini

September 11th, 2019 1 min read

Na ALEX NJERU

MSHUKIWA wa wizi wa kuku alichomwa hadi kufa huku wenzake wawili wakijeruhiwa vibaya katika kijiji cha Kamutuma kaunti ndogo ya Maara, Kaunti ya Tharaka-Nithi.

Watatu hao, ndugu wawili na mpwa wao, walinaswa jana wakiwa na kuku saba, paketi za unga wa ugali na bidhaa zinginezo zilizokuwa zimeibwa kutoka kwa nyumba ya jirani Jumanne usiku.

Murimi Musika alifariki papo hapo, Dennis Mugendi aliokolewa na polisi na kukimbizwa hadi hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Chuka naye Mwendia Musika akatorokea kichakani akiwa na majeraha ya kukatwa kwa panga.

Ndugu hao wawili walinyweshwa mafuta ya taa kwa lazima na kumwagiwa mengine mwilini kabla moto kuwashwa. Akithibitisha kisa hicho, Naibu Kamanda wa Polisi wa Kaunti eneo la Maara, Bw Johnstone Kabusia alisema kuwa, maafisa wake walipowasili eneo la kisa, mshukiwa mmoja alikuwa ameshaaga dunia na mwingine angali anateketea.

“Tulifanikiwa kuokoa mmoja tukamkimbiza hospitalini,” alisema Bw Kabusia. Aliongeza kuwa polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa hicho huku akionya wakazi dhidi ya kuchukua sheria mikononi mwao.

Wakazi walidai kuwa washukiwa hao watatu wenye umri mchanga wamewahangaisha kwa miaka mingi wakivunja nyumba na kuiba kuku, vifaa vya umeme, vyombo vya jikoni na vyakula.

“Watatu hao walikatiza masomo na kuingilia wizi mchana na usiku, jambo lililowalazimu wakati kusalia nyumbani,” alisema mkazi mmoja, Bw John Kimathi. Mkazi, Bi Sarah Makena alidai kuwa wiki moja iliyopita washukiwa walivunja kanisa moja na kuiba mahindi.