Habari Mseto

Watatu wafariki baada ya malori mawili kugongana na kushika moto

February 11th, 2018 1 min read

Na PIUS MAUNDU

WATU watatu waliaga dunia Ijumaa adhuhuri baada ya magari walimokuwa wakisafiria kugongana na kuwaka moto karibu na mji wa Salama, katika barabara ya Nairobi kuelekea Mombasa.

Mtu mwingine aliyejeruhiwa alikimbizwa hospitalini kutibiwa, alisema Mkuu wa Polisi wa Mukaa Bw Charles Muthui alipothibitisha ajali hiyo.

“Lori moja lililokuwa likisafiri kutoka Nairobi lilipoteza mwelekeo baada ya gurudumu kupasuka. Kutokana na hilo, liligonga lori lingine ambalo lilikuwa likitoka upande wa Mombasa,” alisema Bw Muthui. Magari hayo yaliwaka moto na kuteketea.

Ajali hiyo ilitokea huku watu wengine watatu wakiripotiwa kuangamia eneo la Homabay baada ya gari walimokuwa kugonga trakta la kubeba miwa. Watu hao waliaga dunia papo hapo. Licha ya hatua za serikali kidhibiti ajali za barabarani, bado watu wanaendelea kuangamia kutokana na ajali mbaya.