Watatu wahofiwa kufariki katika ajali ya boti Lamu

Watatu wahofiwa kufariki katika ajali ya boti Lamu

NA KALUME KAZUNGU

WAVUVI watatu hawajulikani walipo baada ya mashua waliyokuwa wakisafiria kusombwa na mawimbi makali baharini eneo la Tenewi, Kaunti ya Lamu.

Wavuvi hao walikuwa wamesafiri kutoka Ngomeni, Kaunti ya Kilifi kuingia Lamu kwa shughuli za uvuvi pale ajali ilipotokea siku ya Jumamosi majira ya saa mbili usiku.

Akithibitisha ajali hiyo, Afisa wa Bodi ya Ukaguzi wa Vyombo vya Baharini (KMA), kaunti ya Lamu, Alexander Munga, alisema wawili kati ya wavuvi hao watano walinusurika baada ya kuogelea hadi nchi kavu.

Bw Munga alisema wawili hao kwa sasa wako hali shwari eneo la Mpeketoni.

Alisema KMA kwa ushirikiano na Maafisa wa bodi ya kudhibiti rasilimali za baharini-Kenya Coast Guard (KCGS) tayari wanaendeleza msako wa kuwatafuta watatu waliotoweka baada ya ajali hiyo.

Alisema mashua ya wavuvi hao pia haijapatikana tangu ajali ilipotokea.

“Kuna wavuvi watatu kati ya watano ambao hadi sasa hawajulikani waliko baada ya boti yao kupigwa na dhoruba na kuzama baharini eneo la Tenewi. KMA kwa ushirikiano na KCGS inaendeleza msako wa watatu waliotoweka. Tutawajulisha habari zaidi endapo tutawapata watatu hao. Msako unaendelea,” akasema Bw Munga.

Afisa huyo aidha aliwatahadharisha watumiaji wa bahari kuwa waangalifu msimu huu ambapo Bahari Hindi imekuwa ikishuhudia mawimbi makali na upepo.

“KMA tayari imetoa maonyo mara kadhaa kwa wavuvi na mabaharia wengine kuwa waangalifu hasa miezi hii ya Julai ba Agosti. Bahari mara nyingi imekuwa ikichafuka. Tutii maonyo hayo,” akasema Bw Munga.

Wakati huo huo, wavuvi wa Lamu wameilaumu serikali kwa kutoweka mikakati kabambe ya kukabiliana na majanga ya baharini kila mara yanapotokea.

Mwenyekiti wa wavuvi, kaunti ya Lamu, Mohamed Somo, anasema wavuvi wengi wamekuwa wakipoteza maisha punde ajali zitokeapo kutokana na kukosekana wa kuwaokoa.

“Tulitarajia ajali ya Jumamosi usiku kwamba waokoaji wafike pale siku hiyo hiyo. Cha kusikitisha ni kwamba vikosi vya KMA na KCGS vimefika eneo la tukio leo asubuhi. Haya ni makosa makubwa. Lazima kuwe na mikakati dhabiti ya kuokoa maisha,” akasema Bw Somo.

Ajali ya boti Jumamosi inajiri mwezi mmoja baada ya mabaharia saba kutoka Tanzania kuokolewa pale boti walimokuwa wakisafiria iliposombwa na mawimbi makali na kuzama eneo la Shanga, kaunti ya Lamu.

Saba hao walikuwa wametoka Dar es Salaam, Tanzania kuelekea Kismayu nchini Somalia kuchukua mzigo wa vuma vikuukuu pale ajali ilipotokea majira ya saa nne usiku.

You can share this post!

Sitishwi na jeshi la wanaonipinga – Ruto

Wamaasai wataka operesheni Laikipia isitishwe