Habari

Watatu wanusurika baada ya lori kuanguka Thika Superhighway

June 13th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

WATU watatu Jumamosi wamenusurika kifo baada ya lori la kusafirisha kokoto na vifaa vya ujenzi kuanguka eneo la Carwash katika barabara kuu ya Thika Superhighway.

Watatu hao ni dereva na wasaidizi wake wawili.

Kulingana na walioshuhudia ajali hiyo iliyofanyika eneo la Carwash, kati ya mtaa wa Rosyambu na Githurai, lori hilo lenye nambari za usajili KCH 364T, lilikuwa katika mwendo wa kasi.

“Inaonekana breki zilikataa kufanya kazi, likapoteza mwelekeo wa barabara,” mmoja wa wahudumu wa bodaboda Carwash akaambia Taifa Leo.

Aidha, lori hilo lililokuwa limebeba kokoto lilikuwa katika barabara ya kasi. Liling’oa vyuma vya kando ya barabara na kuanguka katika mtaro wa majitaka ulio kati ya barabara ya kasi na ya nje inayotumika kuchukua na kushusha abiria, ikiwa ni pamoja na magari kutoka Thika Superhighway na kuingia.

Vilevile, tangi la mafuta, gurudumu la kulia la mbele na kioo cha mbele, vyote vilitoka.

“Alichokifanya cha busara dereva huyo ni kujaribu kuliondoa katika barabara ya kasi. La sivyo ingekuwa hasara ya maafa na majeraha mabaya, ikizingatiwa kuwa barabara hii magari huenda kwa mwendo wa kasi,” akasema dereva mmoja wa basi linalohudumu katika barabara hiyo.

Maafisa wa Halmashauri ya Barabara Kuu Nchini, ndiyo KeNHA, waliofika wamewataka watumizi wa barabara hiyo wawe waangalifu, wakihimiza madereva kupunguza kasi.

Mei 2020 kulikuwa na ajali nyingine iliyohusisha lori la mizigo mitaa chache kutoka katika tukio la Jumamosi.

Ni mwezi huo huo ambapo mwanamuziki wa nyimbo za Benga za jamii ya Agikuyu Jimmy Walter maarufu kama Jimmy Wayuni aliangamia katika ajali eneo la Kahawa Sukari, karibu na Chuo Kikuu cha Kenyatta, KU..

Visa vya ajali Thika Superhighway vinaendelea kuongezeka, uendeshaji wa magari kwa mwendo wa kasi na kubadilisha leni bila uangalifu ukitajwa kama kiini kikuu cha mikasa ya ajali.