Watavuruga hesabu za Raila, Ruto?

Watavuruga hesabu za Raila, Ruto?

Na LEONARD ONYANGO

MUUNGANO wa viongozi wa Vuguvugu la Umoja wa Mlima Kenya (MKUF) na vinara wa One Kenya Alliance (OKA) unatishia kuvuruga hesabu za kinara wa ODM Raila Odinga na Naibu wa Rais William Ruto 2022.

Wadadisi wanasema muungano huo utatoa ushindani mkali kwa Bw Odinga na Naibu Rais Ruto katika Uchaguzi Mkuu ujao.Jumanne, vinara wa OKA Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Gideon Moi (Kanu), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na mbunge wa zamani wa Lugari, Cyrus Jirongo walikutana na viongozi wa MKUF wanaoongozwa na aliyekuwa waziri wa Sheria, Martha Karua kuzungumzia muungano mpya.

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo na mbunge wa zamani wa Tetu, Ndung’u Gethenji.Baada ya mkutano huo, viongozi hao walibuni kikosi cha kuoanisha manifesto za OKA na MKUF na kisha kuandaa mwongozo utakaotumiwa kuteua mwaniaji wao wa urais.

Mahojiano yaliyofanywa na Taifa Leo yalibaini kuwa, huenda muungano huo ukateua Bw Mudavadi kuwa mwaniaji wa urais na Bi Karua mwaniaji mwenza.Wadadisi wanasema muungano huo huenda ukasababisha Bw Odinga na Dkt Ruto kukosa kufikisha asilimia 50 na zaidi ya kura, hivyo kulazimisha marudio ya uchaguzi wa urais. Kulingana na mbunge wa Nambale, Bunyasi Sakwa, muungano kati ya OKA na MKUF utakuwa tishio kwa Bw Odinga na Dkt Ruto katika kinyang’anyiro cha urais mwaka ujao.

“Watu wanasema ni farasi wawili watakuwa katika Uchaguzi Mkuu ujao – hilo si kweli. Bado kuna nafasi ya kubuniwa kwa muungano utakaoteua mwaniaji wa urais atakayetoa ushindani mkubwa kwa Ruto na Raila,” anasema Bw Sakwa.

Mbunge huyo wa ANC anasema muungano huo utasababisha kura milioni 4.6 za eneo la Mlima Kenya kugawanywa katika vikapu vitatu hivyo kuvuruga hesabu ya Dkt Ruto.Japo Bw Sakwa anakiri Bw Odinga angali na uungwaji mkono katika eneo la Magharibi, anashikilia kwamba Bw Mudavadi atanyakua karibu asilimia 60 ya kura katika eneo hilo.

Wadadisi wanasema Dkt Ruto anahitaji kupata angalau asilimia 90 ya kura za eneo la Bonde la Ufa na Mlima Kenya ili kuongeza uwezekano wa kushinda urais.Dkt Ruto na Bw Odinga wametangaza nia yao ya kuchukua wawaniaji wenza kutoka Mlima Kenya kwa lengo la kujizolea idadi kubwa ya kura katika eneo hilo.

Bw Sakwa pia anasema muungano huo utapunguza kwa kiasi kikubwa kura za Bw Odinga na Dkt Ruto katika maeneo ya Ukambani, Pwani na Nairobi.Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kufuatilia Utawala katika Serikali za Kaunti, County Governance Watch, Bw Kevin Osido, anasema kuwa, muungano huo utakuwa tishio tu endapo utapata baraka za Rais Uhuru Kenyatta.

Aidha, anasema viongozi wa muungano wa OKA na MKUF watahitajika kufanya mengi kukubalika katika ngome zao ili kuwa tishio kwa Bw Odinga na Dkt Ruto.“Kuungana tu hakutoshi, bali viongozi hao wanastahili kuhakikisha wanakuwa na ushawishi mkubwa katika ngome zao.

Bw Mudavadi, kwa mfano, anafaa kuhakikisha kuwa anajipatia zaidi ya asilimia 80 ya kura katika eneo la Magharibi.“Bw Odinga ameamua kupitia kwa magavana; Bi Charity Ngilu (Kitui), Dkt Alfred Mutua (Machakos) na Prof Kivutha Kibwana (Makueni) kujitafutia uungwaji mkono katika eneo la Ukambani.

Bw Musyoka atakuwa na kibarua kikubwa kukabiliana na ushawishi wa magavana hao watatu,” anasema Bw Osido.Anasema muungano huo ukipata ushawishi mkubwa katika ngome zao, watanyima Bw Odinga na Dkt Ruto asilimia 50 na zaidi ya kura na kulazimisha marudio ya uchaguzi.

“Uchaguzi ukirudiwa, mwaniaji atakayeungwa na muungano huo ndiye ataibuka mshindi na watakuwa wamefanikiwa kuingia serikalini,” anasema Bw Osido.Wandani wa kinara wa Amani National Congress Bw Mudavadi tayari wamesajili muungano unaojulikana kama Kenya Kwanza Alliance (KKA) ambao huenda ukameza OKA na MKUF.

Wakili na Mtaalamu wa Masuala ya Utawala, Javas Bigambo, hata hivyo, amepuuzilia mbali vuguvugu la (MKUF) akisema kuwa linajumuisha wanasiasa wasiokuwa na ushawishi katika eneo la Mlima Kenya.“Vuguvugu la MKUF halijaonekana likipigania masilahi ya watu wa Mlima Kenya kwa vyovyote vile.

Viongozi hao hawawezi kudai kwamba wanazungumza kwa niaba ya watu wa Mlima Kenya ilhali hawajapata idhini ya wakazi wa eneo hilo,” anasema.Bw Bigambo anasema MKUF limejitenga kama kundi linalopigania maslahi ya watu wa Mlima Kenya pekee hivyo itakuwa vigumu mwaniaji wake kukubalika katika maeneo mengine ya nchi.

“Kuna hatari kwamba, mipango ya kuunganisha OKA na kundi la MKUF huenda ikasambaratika Uchaguzi Mkuu wa 2022 ukikaribia. Hawajakuwa wakizunguka nchini kujipigia debe ikilinganishwa na Bw Odinga na Dkt Ruto,” akasema.

Aliyekuwa mbunge wa Mukurweini Kabando wa Kabando anashikilia kuwa kinyang’anyiro cha urais 2022 kitakuwa baina ya farasi wawili; Bw Odinga na Dkt Ruto.“Raila tayari ameidhinishwa na Rais Kenyatta hivyo sioni kwamba atabadili msimamo wake na kuunga mkono muungano wa OKA na MKUF,” anasema.

You can share this post!

Raila kushiriki NDC ya Wiper

Mwatate FC yajipanga kupanda ngazi ligi kuu ya FKF licha ya...

T L