Habari Mseto

Wateja wa Safaricom kuumia zaidi

October 18th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Wateja wa Safaricom watalipa zaidi kutumia huduma za simu ikiwemo ni pamoja na kupiga simu, kutuma ujumbe mfupi na kutumia intaneti.

Hii ni kutokana na ongezeko la ushuru wa asilimia 15 uliotozwa huduma za simu na intaneti kupitia kupitishwa kwa Sheria ya Fedha ya 2018.

Katika taarifa, Safaricom ilisema kuwa imeongeza ada ya kupiga simu kwa senti 30. Kutuma ujumbe mfupi sasa kutagharimu senti 10 zaidi.

Ada hizo mpya zilianza kutumika Jumatano saa sita za usiku. Safaricom imeungana na Zuku na Jamii Telecommunications (JTL) katika kutekeleza ongezeko hilo la bei.

“Zaidi, tumetathmini bei yetu ya masalio ya intaneti, na WIFI ili kuambatana na ushuru huo mpya,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa Safaricom Bob Collymore.

Ushuru huo uliongezwa kutoka asilimia 10 hadi 15, zaidi ya ushuru wa VAT wa asilimia 16 kwa huduma za simu.