Habari Mseto

Wateja wa StandChart kuanza kutoa Sh80,000 kwa ATM

January 11th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Wateja wa benki ya Standard Chartered watanufaika baada ya usimamizi wa benki hiyo kuamua kuongeza kiwango cha fedha wanachoweza kutoa kwa ATM.

Kuanzia mwezi Februari, wateja watakuwa na uwezo wa kutoa Sh80,000 kwa ATM, mara mbili kiwango cha sasa.

Kulingana na benki hiyo, mahitaji ya wateja wake yamegeuka na hatua hiyo ni katika kuwatimizia mahitaji yao.

Kiwango cha juu zaidi kwa sasa ni Sh40, 000 (Gold), Sh50, 000 (Platinum) na Sh60, 000 (Infinite).

Msimamizi wa huduma za kibinafsi za benki Dickson Sitei katika notisi Januari 7 aliwataka wateja wengine wanaotaka kiwango kingine cha mwisho kuwasiliana na benki  katika muda wa siku 30.

“Kiwango cha sasa cha juu zaidi kitaanza kutekelezwa Februari 1 na vitakuwa kwa sarafu ya humu nchini au nje,” alisema.

Kiwango cha juu zaidi unachoweza kupata kupitia kwa ATM kwa benki nyingi nchini ni Sh40, 000.