Habari

Watekaji nyara wachinja mtoto wakitaka Sh50,000

June 2nd, 2019 2 min read

NA BENSON AMADALA

HALI ya huzuni imetanda katika kijiji cha Shitungu, Kaunti ya Kakamega baada ya mwili wa mtoto mwenye umri wa miaka tisa aliyetoweka siku mbili zilizopita, kupatikana katika kichaka akiwa amefariki.

Saida Rajab, mamake marehemu alisema mwanawe Ismaili Shukkar aliondoka nyumbani Jumamosi akielekea katika msikiti moja mjini Kakamega kwa mafunzo ya Madrasa lakini hakurejea.

Hata hivyo, aliingiwa na wasiwasi watu wasiojulikana walipompigia simu wakitaka kulipwa Sh50,000 kabla ya kumwaachilia mwanawe. Imebainika mshukiwa ambaye alionekana mara ya mwisho na marehemu tayari amenyakwa na polisi ili kuhojiwa.

Kamanda wa Polisi wa Kakamega Wlikister Verah alisema alipokea taarifa kuhusu tukio hilo na maafisa wake tayari wameanzisha uchunguzi kulihusu, wakilenga kuwakamata waliomuua mtoto huyo.

“Mamake mtoto huyo aliripoti kisa hicho kwa polisi baada ya kupigiwa simu na mwanaume aliyeitisha Sh50,000 kama kiokozi ili kumwaachilia mtoto huyo. Cha kusikitisha ni kwamba amepatikana ameuawa. Tayari tumemnasa mshukiwa ambaye tunaendelea kumhoji,” akasema Bi Verah.

Polisi wakibeba mwili wa mtoto wa miaka tisa aliyeuawa kichakani kijijini Shikhungula, Kakamega. Picha/ Isaac Wale

Hata hivyo, wanakijiji wa Shitungu wamelalamika kwamba haya yalikuwa mauaji ya pili katika kipindi siku 30 baada ya mwili wa mwanamke pia kupatikana ndani ya kichaka hicho.

Wavamizi walidaiwa kukata kichwa cha mwanamke huyo kisha kuutelekeza mwili wake kwenye kichaka hicho, hali ambayo sasa imewasababishia wenyeji hofu kubwa kuhusu usalama wao.

Wakiwa wamejawa na hasira, wanakijiji hao walimlaumu chifu na wazee kwa kufeli kutatua ukosefu wa usalama unaoendelea kushuhudiwa eneo hilo.

“Tunawaomba polisi na Kamishina wa Kaunti kuingilia suala hili. Wahalifu hao wanajificha kichakani kisha kuwavamia wanafunzi wanaoenda au kurudi kutoka shuleni na pia akina mama. Utovu huu wa usalama unafaa kushughulikiwa haraka ili kuyaokoa maisha,” akasema mwanakijiji.

Akizungumza katika eneo la tukio, Kamanda wa Polisi wa Kakamega ya Kati David Kabena alieleza kusikitishwa kwake na jinsi mvulana huyo alivyochinjwa.

“Wahalifu hao walimchinja kinyama shingoni kisha kuutupa mwili wake kwenye kichaka. Aliuawa vibaya sana. Tunaendelea kuzidisha doria kuwakamata wahalifu hawa ili wakabiliwe kwa sheria kortini,” akasema Bw Kabena.