Habari za Kaunti

Waliopata kazi za mjengo watetea mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu

January 23rd, 2024 2 min read

NA TITUS OMINDE

VIBARUA, wajenzi, wanakandarasi miongoni mwa watu wengine ambao wamenufaika na mradi wa nyumba za bei nafuu unaoendelea Uasin Gishu, walitetea mradi huo vikali wakati wa ushirikishwaji wa umma kuhusu Mswada wa Nyumba za bei Nafuu 2023 uliofanyika mjini Eldoret mnamo Jumatatu.

Wengi wa washiriki kutoka Kaunti Ndogo sita za Uasin Gishu, ambapo mradi huo tayari umezinduliwa, walipongeza mradi huo.

“Tangu mradi huu uanze katika mtaa wa Kidiwa katika kaunti ndogo ya Turbo, nimepata ajira kama mfanyakazi wa kawaida. Ndiyo maana ninaunga mkono mswada huo na kuwaomba wanaoupinga waachane na siasa ambazo zinaumiza mahasla kama mimi,” akasema Bw David Mutsemi, mmoja wa wafanyakazi wa kawaida katika eneo hilo.

Hata hivyo, aliitaka serikali kuangalia upya pendekezo la kulipa asilimia 10 kabla ya kumiliki nyumba lengwa huku akisema kuwa itakuwa vigumu kwa watu wa tabaka la chini kupata pesa zinazohitajika kumiliki nyumba hizo.

“Serikali inahitaji kuangalia upya asilimia hiyo na kuweka aslimia afueni kwa watu wa matabaka ya chini kama sisi, asilimia kumi ni ghali sana kwa Wakenya wa kawaida kama mimi,” alisema Bw Mutsemi.

Wabunge kutoka Uasin Gishu wakiongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Kike Gladys Boss Shollei, waliwataka wakazi kulinda mradi huo kwa njia zote kwa kupinga wale wanaopinga mradi huo kupitia mahakama.

“Watu ambao wameenda kortini kusimamisha mradi huu si miongoni mwa wanufaika. Ninyi kama wanufaika ungeni serikali mkono kwa hali na mali ili kuona kwamba mradi huu unafaulu,” alisema Bi Shollei.

Alisema mradi huo haukukusudiwi kumnufaisha Rais William Ruto bali Wakenya wa mapato ya chini.

Mbunge wa Moiben Phillis Bartoo, alitoa changamoto kwa wakazi wa Moiben kuunga mkono mradi huo bila kujali wale ambao wanaupinga kupitia kwa mahakama.

“Ushiriki huu wa umma sio tukio la kujionyesha na kujipendekeza tu kwa umma. Ni utaratibu wa sheria kama ilivyoelekezwa na mahakama na tunahitaji kuwapa Wakenya fursa ya kutoa maoni yao kuhusu swala hili,” akasema Bi Bartoo.

Viongozi wengine wa eneo hilo waliopongeza mradi huo ni pamoja na Gavana Jonathan Bii, Seneta Jackson Mandago, na mbunge wa Kesses Julius Ruto.

Waliunga mkono mradi huo wakiwataka wenyeji kuunga mkono kwa kila hali.