HabariSiasa

Watetezi kimya Jubilee ikitatiza demokrasia, haki

November 26th, 2019 2 min read

KIMYA cha Wakenya wakati mafanikio ya demokrasia yanapoendelea kutatizwa na utawala wa Jubilee kimezua wasiwasi wa nchi kurudi katika utawala wa kidikteta.

Hii ni baada ya utawala wa Rais Uhuru Kenyatta kuendelea kuhujumu taasisi kuu za kulinda demokrasia zikiwemo bunge, upinzani, mashirika ya kijamii, vyombo vya habari na mahakama.

Baada ya Rais Kenyatta, Raila Odinga na Kalonzo Musyoka kutuliza ushindani wao wa kisiasa na kuanza kushirikiano, Bunge limekuwa kikaragosi cha Serikali Kuu kwa kupitisha kila kitu inachotakiwa kuidhinisha.

Hii ni baada ya wabunge wa upinzani kuanza kupiga ngoma moja na wenzao wa chama tawala cha Jubilee.

Upinzani nao ulizamishwa baada ya handisheki wakati vigogo Odinga wa ODM na Bw Musyoka wa Wiper walipopata vyeo, hali iliyowapofusha kuhusu maslahi ya wananchi ambayo walikuwa wakidai kutetea.

Mashirika ya kijamii nayo yalizimwa kwa sheria kali ambazo zililemaza shughuli zao pamoja na kukosa ufadhili.

Pia baadhi ya wanaharakati waliokuwa wakiegemea upinzani walinyamaza wakati Bw Odinga na Bw Musyoka walipomezwa na Jubilee.

Navyo vyombo vya habari vimelemazwa hasa kifedha kwa kukosa matangazo kutoka kwa serikali na hali ngumu ya kiuchumi ambayo imetatiza mapato ya kuviwezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Kumekuwepo pia na juhudi za kulemaza mahakama kwa kuingilia utendakazi wake na kukoroga bajeti ya idara hiyo.

Wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Daniel Moi ambao ulitatiza demokrasia, mashirika ya kijamii yakiongozwa na wanaharakati machachari yaliungana na vyombo vya habari kumaliza utawala wa chama kimoja na kuweka nchi kwenye mkondo wa kukua kidemokrasia.

Lakini wakati huu ambapo mafanikio hayo yanaendelea kuzimwa na Jubilee pamoja na uchumi kuzorota, hakujakuwa na wanaharakati wa kushinikiza kuheshimiwa kwa demokrasia na haki kwa Wakenya.

Hii ni kinyume na miaka ya tisini ambapo viongozi kama Seneta James Orengo, Prof Anyang Nyong’o, Marehemu Wangari Maathai, Kaasisi Timothy Njoya, Paul Muite, Gitobu Imanyara, aliyekuwa Jaji Mkuu Dkt Willy Mutunga, Bw Njeru Kathangu, Bw Koigi wa Wamerere na wakili Gibson Kamau Kuria waliongoza juhudi za kuleta demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa.

Wanaharakati hawa wamekuwa kimya demokrasia waliyopigania ikihujumiwa na Jubilee isipokuwa Bi Martha Karua ambaye amekuwa akisikika akiikosoa serikali.

“Ni Bi Karua pekee ameonyesha msimamo wa kweli kuwatetea wananchi lakini sauti yake pekee haitoshi. Anahitaji usaidizi wa wanaharakati wengine ili kujaza nafasi ya ukosefu wa upinzani nchini,” asema mchanganuzi wa siasa Bw Wycliffe Muga.

Baadhi ya wadadisi wanasema kimya chao kinatokana na umri wao mkubwa na wengine kujiunga na serikali.Pia viongozi wengi walitosheka na kushawishiwa kwa “minofu” waliyopata baada ya kujiunga na serikali.

Wadadisi wanawataja baadhi ya viongozi hao kama wasaliti, hasa baada ya Bw Odinga kujiunga na Rais Kenyatta kwenye handisheki.Wanasema kuwa sauti ya viongozi hao ingekuwa muhimu wakati kama huu Wakenya wanapoteseka.

Hata baada ya wao kuzeeka ama kumezwa na serikali, kumekosekana wanaharakati wachanga wa kuongoza juhudi za kulinda haki na demokrasia.

Ni mwanaharakati Boniface Mwangi pamoja na kikundi cha Haki Afrika kikiongozwa na Hussein Khalid ambao wamesikika wakipinga utawala wa Rais Kenyatta kila mara unapokiuka sheria ama kuchukua hatua za kunyanyasa Wakenya.