Michezo

Watford, Brighton na Villa wataka EPL ichezewe nyumbani

May 10th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WATFORD imekuwa klabu ya tatu baada ya Brighton na Aston Villa kupinga matumizi ya viwanja visivyokuwa vya nyumbani kwa kikosi chochote kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) zitakaporejelewa msimu huu.

Mwenyekiti wa Watford, Scott Duxbury amesema kwamba hatua hiyo itayeyusha hadhi na usawa katika kipute hicho kinachojivunia ufuasi mkubwa duniani.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, vikosi vya EPL havitarajiwi kupiga kura ya iwapo mechi zilizosalia muhula huu zitapigiwa katika viwanja visivyokuwa vya nyumbani kwa klabu yoyote kati ya 20 zitakazoshirikishwa kikao cha Mei 11, 2020.

Badala yake, kikao hicho kinatazamiwa kujadili suala la iwapo mikataba ya baadhi ya wachezaji iliyokuwa itamatike mwishoni mwa Juni itarefushwa na klabu husika hadi kampeni zote za msimu huu zitamatike.

Kwa kuwa vikosi vitatu tayari vimepinga mapendekezo ya mechi hizo kutochezewa nyumbani kwa klabu yoyote, inaaminika kwamba timu nyingi kati ya 17 nyinginezo zitaunga mkono hatua ya Watford, Brighton na Villa.

Kabla ya mwafaka kuhusiana na suala hilo kupatikana, vinara wa soka ya Uingereza watakuwa pia wakitarajia mwongozo wa serikali kuhusu namna ya kudumisha hali ya usalama na kuwadhibiti baadhi ya mashabiki watundu watakaovunja kanuni zilizopo za afya na kutaka kuingia viwanjani kutilia shime klabu zao.

Mwongozo huo unatazamiwa kutolewa na Waziri Mkuu Boris Johnson mnamo Mei 11.

“Bila shaka hakuna jinsi ambavyo tutakuwa na mashabiki uwanjani. Hata hivyo, inasikitisha zaidi kuambiwa kwamba hatutaweza kusakata mchuano wowote katika uwanja wetu wa nyumbani wa Vicarage Road ambao tumeuzoea ili tuchume nafuu ya utulivu unaotokana na uelewa huo,” akasema Duxbury.

Kivumbi cha EPL kilisimamishwa kwa muda usiojulikana mnamo Machi 13 kutokana na janga la corona. Kufikia sasa, ipo mipango ya ligi hiyo kurejelewa kuanzia Juni 12 na vikosi husika tayari vimeanza maandalizi ya kukamilisha raundi tisa za mechi zilizosalia.

Nchini Ujerumani, Ligi Kuu ya Bundesliga imeratibiwa kuendelezwa kuanzia Mei 16 na kila kikosi kitakuwa na fursa ya kusaka gozi katika uwanja wake wa nyumbani bila mashabiki.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Ligi Kuu za soka ya bara Ulaya, Richard Bevan ameonya kwamba huenda kipute cha EPL msimu huu kikafutiliwa mbali iwapo klabu hazitaafikiana kuhusu pendekezo la mechi zilizosalia kutosakatiwa nyumbani kwa kikosi chochote.

Japo kila timu ingalikuwa na wajibu wa kudhibiti mashabiki wake wa nyumbani na kulaumiwa kwa matukio yoyote ya utovu wa nidhamu, Bevan anahisi kwamba itakuwa mzigo zaidi kwa maafisa wa usalama kufanikisha uendeshaji wa mechi zilizobaki muhula huu.

Uwanja wa London unaomilikiwa na West Ham United, Emirates wa Arsenal na Etihad wa Manchester City ni miongoni mwa viwanja ambavyo tayari vimependekezwa na washikadau kutumiwa kuandaa michuano yote iliyosalia muhula huu.

Viwanja vingine vinavyotarajiwa kuidhinishwa baada ya maafisa wa usalama kutathmini usalama wao ni Amex (Brighton), St Mary’s (Southampton), King Power (Leicester City), Villa Park (Aston Villa), Old Trafford (Man-United) na uwanja wa kitaifa wa Wembley jijini London.