Michezo

Watford sasa wapata kocha mrithi wa Pearson

August 16th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

WATFORD wamempokeza Vladimir Ivic, 43, mikoba yao ya ukocha kwa mkataba wa mwaka mmoja. Kandarasi hiyo itarefushwa kutegemea matokeo yatakayosajiliwa na kikosi hicho cha Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) chini yake.

Ivic ambaye ni kocha wa zamani wa Maccabi Tel Aviv ya Israel anamrithi mkufunzi Nigel Pearson aliyetimuliwa na Watford zikiwa zimesalia mechi mbili pekee kwa kampeni za msimu huu wa 2019-20 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kukamilika rasmi.

Licha ya Pearson kupigwa kalamu wakati ambapo Watford walikuwa wakipigania nafasi finyu ya kusalia EPL, kikosi hicho kiliteremshwa ngazi baada ya kupoteza mechi zote mbili chini ya kocha mshikiliz Hayden Mullins.

Kichapo cha 3-2 walichopokezwa na Arsenal katika siku ya mwisho ya msimu kilitamatisha kipindi cha miaka mitano ya Watford waliotinga fainali ya Kombe la FA mnamo 2019 kunogesha kipute cha EPL.

Ivic hana tajriba yoyote katika soka ya Uingereza ama akiwa mchezaji au kocha japo Watford wamesisitiza kwamba wameridhishwa na mbinu zake za ukufunzi.

“Ni mara yangu ya kwanza nchini Uingereza na itanilazimu kuzoea mazingira haya mapya haraka iwezekanavyo kisha nijitahidi kurejesha Watford kwenye EPL,” akasema Ivic aliyewahi kuvalia jezi za timu ya taifa ya Serbia katika siku zake za usogora.

Ujio wake ugani Vicarage Road kunamfanya kocha wa nne wa Watford katika kipindi cha miezi 12 baada ya kutimuliwa kwa Javi Gracia na Quique Sanchez Flores mwanzoni mwa msimu huu. Kuondoka kwa wawili hao kulimpisha Pearson kuingia Watford mnamo Disemba 2019.

Ivic alisalia huru baada ya kuwaongoza Maccabi Tel Aviv kunyanyua mataji mawili ya Ligi Kuu ya Israel. Awali, alikuwa amedhibiti pia mikoba ya PAOK FC aliowanyanyulia ubingwa wa Greek Cup.

Ametua Watford pamoja na makocha watatu waliokuwa wasaidizi wake kambini mwa Maccabi Tel Aviv.