Michezo

Watford wamfuta kazi mkufunzi Ivic na sasa wanatafuta kocha wa tano chini ya mwaka mmoja

December 20th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

WATFORD wamemfuta kazi kocha Vladimir Ivic baada ya kudhibiti mikoba ya kikosi chao kwa kipindi cha miezi minne pekee.

The Hornets ambao wameshinda mechi tisa kati ya 20 zilizopita kwenye Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) msimu huu, wanashikilia nafasi ya tano jedwalini kwa alama nne nyuma ya nambari mbili Bournemouth na tisa nyuma ya viongozi Norwich City.

Ivic, 43, alitia saini mkataba wa mwaka mmoja kambini mwa Watford mnamo Agosti 2020 baada ya kuaminiwa kuwa mrithi wa mkufunzi Nigel Pearson aliyefutwa kazi siku chache kabla ya kikosi hicho kuteremshwa ngazi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika msimu wa 2019-20.

Kutimuliwa kwa Ivic kunamaanisha kwamba Watford kwa sasa wanatafuta kocha wa tano chini ya kipindi cha mwaka mmoja.

Kufurushwa kwa Ivic ambaye ni raia wa Serbia kunajiri siku moja baada ya Watford kupokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Huddersfield ugenini. Kichapo hicho kilikuwa cha pili kwa Watford kupokea kutokana na mechi 11 ambazo pia zimewashuhudia wakiambulia sare mara nne.

Ivic alimpumzisha nahodha wa Watford, Troy Deeney katika mechi hiyo licha ya fowadi huyo matata kufunga katika kila mojawapo ya mechi tatu za awali za waajiri wake.

Licha ya Troy kupangwa kwenye kikosi cha wachezaji wa akiba dhidi ya Huddersfield, Ivic hakumleta uwanjani sogora huyo hata dalili zote zilipoashiria kwamba Watford walikuwa wanapoteza mechi hiyo.

Katika mahojiano yake na wanahabari, Ivic alisisitiza kwamba hatua yake hiyo ilichochewa na “utovu wa

Watford kwa sasa wanapania kuajiri kocha wa tano tangu mwanzoni mwa kampeni za msimu uliopita wa 2019-20.

Javi Gracia alitimuliwa mnamo Septemba 2019 na nafasi yake kutwaliwa na mkufunzi wa zamani wa Watford, Quique Sanchez Flores aliyerejea uwanjani Vicarage Road.

Watford wakiwa mkiani mwa jedwali la EPL, Flores alifutwa kazi baada ya kuongoza kikosi hicho kushinda mechi mbili pekee kutokana na 12. Kuondoka kwake kulimpisha Pearson aliyepokezwa mikoba ya ukocha mnamo Disemba 2019.

Mbali na kuwanyanyua Watford na kuwaondoa katika mduara wa vikosi vitatu vya mwisho vilivyokuwa katika hatari ya kuteremshwa ngazi EPL, Pearson aliwaongoza waajiri wake kuwapokeza mabingwa Liverpool kichapo chao cha kwanza cha msimu (3-0) katika mchuano wa ligi uliosakatiwa uwanjani Vicarage Road mnamo Februari 29.

Chini ya kocha mshikilizi Hayden Mullins, Watford walipoteza mechi mbili za mwisho wa msimu wa 2019-20 na kuteremshwa daraja kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha misimu mitano kwenye EPL.

Tangu Juni 2012 ambapo umiliki wa Watford ulitwaliwa na familia ya Pozzo kutoka Italia ambayo pia inamiliki vikosi vya Udinese na Granada nchini Italia na Uhispania mtawalia, Watford wamebadilisha makocha mara 13.

Miongoni mwa wakufunzi waliohudumu kambini mwa kikosi hicho kwa kipindi kifupi zaidi ni Oscar Garcia aliyedhibiti mikoba kwa siku 27 pekee mnamo Septemba 2014 kabla ya kujiuzulu kutokana na matatizo ya afya.

Billu McKinlay aliyejaza nafasi yake alihudumu uwanjani Vicarage Road kwa kipindi cha siku nane pekee ambapo alisimamia mechi mbili kabla ya wamiliki kubatilisha maamuzi ya kumwajiri na badala yake kumpokeza Slavisa Jokanovic mikoba ya ukufunzi.

Ni wakufunzi wawili pekee ambao wamewahi kuhudumu kambini mwa Watford kwa zaidi ya mwaka mmoja chini ya umiliki wa familia ya Pozzo. Hao ni Gianfranco Zola aliyenoa kikosi hicho kati ya Julai 2012 na Disemba 2013 na Javi Gracia aliyewaongoza The Hornets kutinga fainali ya Kombe la FA mnamo 2019. Kocha huyo aliwatia makali vijana wa Watford kati ya Januari 2018 na Septemba 2019.