Michezo

Watford wasajili chipukizi kutoka Ufaransa

April 30th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

WATFORD wamemsajili kiungo Pape Gueye, 21, kwa mkataba wa miaka mitano kutoka kikosi cha Le Harve kinachoshiriki Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Ufaransa (Ligue 2).

Mkataba uliotiwa saini na chipukizi huyo mzawa wa Ufaransa hapo jana utaanza kutekelezwa rasmi kuanzia Julai 1, 2020.

Kandarasi ya sasa kati ya Gueye na Le Havre inatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu. Kusajiliwa kwake na Watford kulichochewa na maamuzi ya kufutiliwa mbali kwa msimu huu mzima katika vipute vya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) na Ligue 2.

Serikali ya Ufaransa imetisha zaidi shughuli zote za michezo nchini humo hadi Septemba 2020 kutokana na virusi vya corona.

Katika taarifa iliyotolewa jana na Watford, kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kilisema kwamba kimeafikiana na Le Havre kuhusu usajili wa Gueye ambaye tayari ametia saini mkataba wa awali huku akisubiri kutua rasmi ugani Vicarage Road mnamo Julai.

Watford almaarufu ‘The Hornets’ kwa sasa wananing’ia pembamba mkiani pa jedwali la EPL kwa alama 27 sawa na West Ham United na Bournemouth ambao kwa pamoja na Aston Villa na Norwich City, wako katika hatari ya kuteremshwa daraja mwishoni mwa muhula huu.

Watford walicheza kwa mara ya mwisho mnamo Machi 7, 2020 dhidi ya Crystal Palace katika mchuano wa EPL uliowashuhudia wakipokezwa kichapo cha 1-0 uwanjani Selhurst Park.

Kivumbi cha EPL kinatarajiwa kurejelewa wakati wowote kuanzia Mei 16 baada ya kuahirishwa mwanzoni mwa Machi 2020 kwa sababu ya mlipuko wa virusi vya homa kali ya corona.