Michezo

Watford wateremshwa ngazi na City

July 22nd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WATFORD kwa sasa wako katika hatari ya kushushwa ngazi katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu iwapo watapoteza mechi yao ya mwisho dhidi ya Arsenal mnamo Julai 26 nao Aston Villa wasajili sare au kuibuka na ushindi dhidi ya West Ham United uwanjani London.

Kichapo pia kutoka kwa Everton kitawateremsha daraja Bournemouth ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya 19 kwa alama 31, tatu nyuma ya Watford na Villa.

Wakicheza dhidi ya Manchester City mnamo Julai 21, 2020 uwanjani Etihad, Watford walipokezwa kichapo cha 4-0 kupitia mabao ya Phil Foden, Aymeric Laporte na Raheem Sterling aliyefunga mawili.

Watford waliongozwa katika mechi hiyo na kocha wao wa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 23, Hayden Mullins ambaye aliaminiwa kushikilia mikoba ambayo kocha Nigel Pearson alipokonywa mnamo Julai 20, 2020. Msaidizi wa Mullins kwa sasa ni Graham Stack aliyekuwa pia msaidizi wa Pearson aliyekuwa kocha wa tatu kufutwa na Watford muhula huu.

Watford walijitosa ugani kwa minajili ya mechi hiyo dhidi ya Man-City wakitarajia kibarua kigumu hasa ikizingatiwa kwamba masogora hao wa kocha Pep Guardiola walikuwa wamewapokeza kichapo cha 8-0 katika mkondo wa kwanza mnamo Septemba 21, 2020.

Nusura Man-City wafungiwe mabao mengine mawili zaidi mwishoni mwa kipindi cha pili kupitia kwa Gabriel Jesus na Kevin De Bruyne ila yakafutiliwa mbali kwa kuotea.

Ushindi huo wa Man-City uliwasaza Watford katika nafasi ya 18 kwenye msimamo wa jedwali.

Wapinzani wa Villa katika mchuano wa mwisho wa EPL msimu huu ni West Ham ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya 16 kwa alama 37. Kikosi hicho cha kocha David Moyes kinahitaji angalau alama moja dhidi ya Manchester United mnamo Julai 22 usiku ili kukwepa shoka ambalo vinginevyo, litawashusha ngazi.

Watford hawajawahi kuwashinda Man-City katika jumla ya mechi 18 zilizopita katika mapambano yote, rekodi ambayo ilianzia Machi 1989. Katika msimu wa 2018-19, Man-City waliwaponda Watford 6-0 katika fainali ya Kombe la FA.

Man-City kwa sasa wanajivunia kuwazidi Watford maarifa katika jumla ya mechi 13 mfululizo na kuwafunga jumla ya mabao 50-6 kutokana na mechi hizo zote.

Pearson ambaye amewahi pia kudhibiti mikoba ya Leicester, anakuwa mkufunzi wa tatu baada ya Javi Gracia na Quique Sanchez Flores kutimuliwa uwanjani Vicarage Road muhula huu.

Pearson alipokezwa mikoba ya Watford mnamo Disemba 2019 kwa matarajio ya kuongoza Watford kutamba katika soka ya Uingereza msimu huu wa 2019-20.

Chini ya ukufunzi wake, Watford walisajili ushindi katika mechi saba za EPL ikiwemo ile iliyowashuhudia wakizamisha chombo cha mabingwa Liverpool kwa mabao 3-0 mnamo Febrauari 29, 2020 uwanjani Vicarage Road. Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kwa Liverpool kupoteza katika kivumbi cha EPL msimu huu.

Mullins aliwahi pia kushikilia mikoba ya kikosi hicho baada ya Sanchez Flores kufutwa kazi mnamo Disemba 2019.

Alisimamia mechi iliyowashuhudia Watford wakipokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Leicester mnamo Disemba 4, 2019 na sare tasa dhidi ya Crystal Palace mnamo Disemba 7, 2019 kabla ya uteuzi wa Pearson kurasimishwa.

Kocha atakayeaminiwa kuwa mrithi rasmi wa Pearson kambini mwa Watford atakuwa mkufunzi wa 13 wa kikosi hicho tangu kuajiriwa kwa Sean Dyche yapata miaka tisa iliyopita.