Michezo

Watford wavunja ndoa na kocha Nigel Pearson

July 20th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WATFORD wamemtimua kocha Nigel Pearson zikisalia mechi mbili pekee kabla ya kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kutamatika rasmi.

Kiini cha kufurushwa kwa Pearson ni matokeo duni ya kikosi hicho ambacho kwa sasa kinashikilia nafasi ya 17 kwa alama 34, tatu pekee mbele ya Aston Villa na Bournemouth ambao pia wapo katika hatari ya kushushwa ngazi mwishoni mwa kampeni za msimu huu baada ya Norwich City.

Pearson ambaye ni amewahi kudhibiti mikoba ya Leicester City, anakuwa mkufunzi wa tatu baada ya Javi Gracia na Quique Sanchez Flores kutimuliwa uwanjani Vicarage Road muhula huu.

Kocha wa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 23, Hayden Mullins atasimamia mechi mbili za mwisho za Watford katika kipute cha EPL msimu huu dhidi ya Manchester City na Arsenal mtawalia. Atashirikiana na Graham Stack ambaye amekuwa msaidizi wa Pearson.

Pearson alipokezwa mikoba ya Watford mnamo Disemba 2019 kwa matarajio ya kuongoza Watford kutamba katika soka ya Uingereza msimu huu wa 2019-20.

Chini ya ukufunzi wake, Watford walisajili ushindi katika mechi saba za EPL ikiwemo ile iliyowashuhudia wakizamisha chombo cha mabingwa Liverpool kwa mabao 3-0 mnamo Febrauari 29, 2020 uwanjani Vicarage Road. Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kwa Liverpool kupoteza katika kivumbi cha EPL msimu huu.

Ingawa hivyo, Watford walipokezwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa West Ham United mnamo Julai 17, 2020. Ni matokeo ambayo yalining’iniza padogo zaidi matumaini yao ya kusalia katika kipute cha EPL msimu ujao hasa ikizingatiwa ugumu wa kibarua kinachowasubiri dhidi ya Man-City na Arsenal wanaolenga kutamatisha kampeni za muhula huu kwa matao ya juu zaidi.

Mullins ambaye ni mkurugenzi wa spoti kambini mwa Watford, aliwahi pia kushikilia mikoba ya kikosi hicho baada ya Sanchez Flores kufutwa kazi mnamo Disemba 2019.

Alisimamia mechi iliyowashuhudia Watford walipokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Leicester mnamo Disemba 4, 2019 na sare tasa dhidi ya Crystal Palace mnamo Disemba 7, 2019 kabla ya uteuzi wa Pearson kurasimishwa.

Kocha atakayeaminiwa kuwa mrithi rasmi wa Pearson kambini mwa Watford atakuwa mkufunzi wa 13 wa kikosi hicho tangu kuajiriwa kwa Sean Dyche yapata miaka tisa iliyopita.

MAKOCHA WA HIVI KARIBUNI WA WATFORD

KOCHA                                   P       W     Pts

Nigel Pearson (2019-20)    20      7      25

Sanchez Flores (2019)         10      1       7

Javi Gracia (2018-19)          56     18     66

Marco Silva (2017-18)         24      7      26

Walter Mazzarri (2016-17)  38    11    40

Sanchez Flores (2015-16)    38    12    45