Michezo

Watimkaji 20,000 kushiriki Beyond Zero

March 7th, 2019 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

ZAIDI ya watimkaji 20,000 wanatarajiwa kushiriki mbio za Beyond Zero Marathon zitakazoandaliwa jijini Nairobi mwishoni mwa wiki hii.

Kwa mujibu wa Jackson Tuwei ambaye ni Rais wa Chama cha Riadha nchini, makala haya ya nne ya mbio hizo yatawajumuisha pia wanariadha wasio na uwezo wa kuona na walioathiriwa kiakili.

Walemavu watapania kutumia mbio hizo kujifua kwa Olimpiki za 2020 zitakazoandaliwa jijini Tokyo, Japan.

Wakimbiaji wazoefu pia watashiriki na kuwania tuzo za haiba katika mbio za kilomita 21 na kilomita 10 zitakazoshuhudia washindi wakitia mfukoni Sh250,000 na Sh100,000 mtawalia.

Margaret Kenyatta ambaye ni mke wa Rais Uhuru Kenyatta, afanya mazoezi na washiriki wengine wakiwemo wanahabari. Picha/ Maktaba

Kulingana na AK, mbio za wanariadha walemavu zitaanza saa kumi na mbili na nusu (6:30a.m.) huku nusu marathon ya kilomita 21 ikianza saa moja kamili (7a.m.).

Baadaye saa mbili na nusu (8:30a.m.), mbio za kilomita 10 zitaanza kabla ya zile za kilomita tatu kufunga ratiba.

“Kutakuwapo pia na matembezi ya kilomita mbili kwa akina mama wajawazito. Kitengo hiki kitalenga kuhamasisha kuhusu umuhimu wa kuzingatia afya wakati wa uzazi,” akasema mratibu wa mbio hizo, Bw Peter Gacheru.

Uchunguzi

Wakati uo huo, AK imeanzisha uchunguzi kuhusu madai ya udanganyifu wa umri miongoni mwa chipukizi watakaoshiriki mashindano ya dunia ya mbio za nyika.

Mwishoni mwa Februari, AK iliteua vikosi vya wanariadha watakaopeperusha bendera ya Kenya kwenye Mbio za Dunia za Nyika zitakazoandaliwa jijini Aarhus, Denmark mnamo Machi 30.

Ingawa hivyo, Paul Mutwii ambaye ni Naibu Rais wa AK amefichua kwamba huenda baadhi ya wanariadha walioteuliwa walishiriki udanganyifu kwa kuwasilisha vyeti ghushi vya kuzaliwa.