Michezo

Watimkaji 4,000 kushiriki Lagos Marathon

January 31st, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

ZAIDI ya wakimbiaji 4,000 kutoka mataifa 58 watatifua vumbi katika makala ya nne ya mbio za Lagos Marathon nchini Nigeria mnamo Februari 2, 2019.

Wakenya David Barmasai Tumo, Jacob Kibet Chulyo, Moses Kigen Kipkosgei, Agnes Jeruto Kiprotich, Caroline Kilel, Georgina Rono na Risper Jemeli Kimayo wako katika orodha hiyo ya washiriki.

Washindi watazawadiwa Sh5,035,000, nambari mbili Sh4,028,000 nao nambari tatu Sh3,021,000. Nambari nne hadi 10 watapokea kati ya Sh2,014,000 na Sh201,400.

Kenya inajivunia mataji matatu katika Lagos Marathon baada ya Abraham Kiptum kushinda kitengo cha wanaume mwaka 2016 na 2017 naye Rodah Jepkorir akaibuka malkia mwaka 2017.

Mfaransa Abraham Kiprotich, ambaye ni mzawa wa Kenya, na Jepkorir wanashikilia rekodi za Lagos Marathon za saa 2:13:04 na 2:37:52 walizoweka mwaka 2018 na 2017, mtawalia. Vyombo vya habari nchini Nigeria vimeripoti kwamba maandalizi yamekamilika, huku wakimbiaji kutoka nje ya nchi hiyo wakianza kuwasili Januari 29.