Habari Mseto

Watoa mwito BBI ihusishe maoni ya vyama kadhaa vya kisiasa

February 6th, 2020 2 min read

Na BRENDA AWUOR

WAWAKILISHI wa vyama vya kisiasa 68 wameahidi kuunga mkono ripoti ya maridhiano (BBI) iwapo itakosolewa.

Kutokana na mkutano baina ya kamati ya vyama vya kisiasa na wawakilishi wa chama cha ODM ulioandaliwa hoteli ya Pinecone, Kisumu, ni dhahiri kwamba vyamba hivi vya kisiasa vinakosoa ripoti ya maridhiano.

Mkutano ulioandaliwa kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuhusu ripoti ya maridhiano, imepitia marekebisho kutoka kwa wawakilishi wa vyama vya kisiasa.

Kwa kutoa malalamishi yao dhidi ya marekebisho, wawakilishi kutoka chama cha Ford Kenya, chama cha uzalendo, chama cha Independent, chama cha Ford Asili, miongoni mwa vingine wametoa sababu kadhaa za haja ya marekebisho.

Bw Julius Wambua, mwakilishi wa chama cha Independent, alisema kuwa ripoti ya maridhiano ni swala la kitaifa na ni lazima ihusishe maoni ya ‘’mwananchi wa kawaida’’ bali haipaswi kuhusisha maoni kutoka kwa viongozi wa vyama viwili tu.

Kwa kurejea ukurasa kwenye ripoti ya maridhiano, alisema kuwa, ripoti imehusisha maoni ya watu elfu saba.

Maoni yake pamoja na ya wawakilishi walioongea ni kuwa, watu hao ni kutoka chama cha ODM na Jubilee pekee kwa kuacha nje maoni ya wanavyama vingine.

“Ripoti ya maridhiano imehusisha maoni ya watu elfu saba kutoka kwa vyama vyenye viongozi wao waliosalimiana huku wakiacha nje maoni kutoka kwa vyama vingine pamoja na wananchi wa kawaida,’’ alieleza.

Bi Jane Njiru, mwakilishi wa chama cha Ford Asili, alipendekeza kuwa vyama vyote ambavyo vimesajiliwa vijumuishwe katika ripoti ya maridhiano, iwapo chama kinaunga mkono BBI au la.

Swala hili iliungwa mkono na wawakilishi wengi huku wakisema kuwa iwapo vyama vyote vitajumuishwa katika ripoti ya maridhiano, wengi wao wataunga mkono ripoti ya maridhiano.

Bi Njiru, alieleza kuwa si jambo sawa vyama viwili kunyakua mali ya serikali na kuitumia vibaya kwa maadai ya kuhamasisha wananchi,huku vyama vingine vikikula kwa macho.

‘’Vyama nyote viwekwe ndani kisha rasilimali pamoja na fedha kugawanywa kwa kila chama,’’ alieleza.

Baadhi ya wawakilishi, walilalama suala ya kupokea ripoti ya maridhiano kwa mara ya kwanza.

Walieleza kuwa, licha ya wao kupokea ripoti hiyo kwa mara ya kwanza ni wazi kuwa mwananchi wa kawaida hajapata kuona wala kusoma ripoti hiyo, huku magavana wakitangaza kuwa wananchi wao wamekubali ripoti.

Mwakilishi wa Ford Kenya, Joe Ruhu pamoja na Saja Philipo wa chama cha Uzalendo walionyesha kuiunga ripoti ya maridhiano huku wakisema kuwa wanaunga mkono ripoti hiyo ila marekebisho kutoka kwa vyama vingine yashughulikiwe.

Mwenyekiti wa kamati ya vyama vya kisiasa, Bw Irungu Wilson, akiongea na wanahabari alieleza kuwa, Jopo la ripoti ya maridhiano lizingatie malalamiko yao kwenye ripoti kabla ya kura ya maoni.

“Tunaomba wanajopo wa ripoti ya maridhiano kujumuisha malalamishi yetu baada ya kukataa katika awamu ya kwanza ndipo iende kwa  hatua ya maoni,’’ alihitimisha.