Habari Mseto

Watoto 282 waliofanya KCPE Laikipia hawajulikani waliko

March 6th, 2019 1 min read

Na STEVE NJUGUNA

KAMISHNA wa Kaunti ya Laikipia, Bw Onesmus Musyoki ameagiza machifu, manaibu wao na wakuu wa shule katika kaunti hiyo wasake watahiniwa 282 waliofanya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) mwaka uliopita lakini hawajajiunga na shule za upili.

Bw Musyoki alisema wanafunzi hao walihitajika kujiunga na shule za upili lakini hawajulikani waliko.

“Wengine wao, hasa wasichana ni wajawazito na haijulikani walikoenda. Serikali tayari imegharamia karo zao na hatutarudi nyuma hadi tuwapate,” akasema jana baada ya kusimamia mkutano wa usalama wa kaunti hiyo.

Alisema serikali imeagiza wanafunzi wenye umri wa chini ya miaka 18 ambao waliamua kujiunga na taasisi za mafunzo ya kiufundi baada ya kufanya KCPE mwaka uliopita, washauriwe kujiunga na shule za upili kwanza.

“Serikali itashikilia msimamo wake kwani lazima tuhakikishe asilimia 100 ya wanafunzi wanaingia shule za upili kutoka shule za msingi,” akasema Bw Musyoki.