Watoto 3 milioni katika kaunti 13 kupokea chanjo ya polio

Watoto 3 milioni katika kaunti 13 kupokea chanjo ya polio

Na WACHIRA MWANGI

KENYA imezindua kampeni ya chanjo ya polio inayolenga watoto 3 milioni walio na umri wa chini ya miaka mitano katika kaunti 13 nchini.

Wizara ya Afya imesema kwamba kampeni hiyo ilianzishwa baada ya virusi vinavyosabisha ugonjwa huo kugunduliwa kaunti za Garissa na Mombasa.

Kaunti zinazolengwa ni Garissa, Isiolo, Kajiado, Kiambu, Kilifi, Kitui, Lamu, Machakos, Mandera, Mombasa, Nairobi, Tana River, Wajir na kambi ya wakimbizi ya Daadab. Katika Kaunti ya Mombasa watoto 250,000 watapatiwa chanjo hiyo

Shughuli ya kutoa chanjo hiyo ilizinduliwa Ijumaa ambapo serikali za Kaunti zitashirikiana na Serikali ya Kitaifa, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO)na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na watoto (Unicef).

Awamu ya kwanza ya chanjo hiyo ilianza Jumamosi na itaendelea hadi Jumatano na awamu ya pili itakuwa kati ya Juni 19 na 23.

Shughuli hiyo ilizinduliwa katika Shule ya Msingi ya Likoni.

Kampeni hiyo itafanyika katika kaunti zinazokaribiana na eneo la Kaskazini Mashariki ambapo kisa cha polio kiliripotiwa mapema mwaka 2021.

“Aina ya polio ilipatikana katika maji taka Mombasa. Kisa kimoja huchukuliwa kuwa mkurupuko kwa sababu virusi huwa vinaenea kwa haraka na ni hatari, hivyo basi kuna haja ya kutoa chanjo,” alisema Afisa Mkuu wa Afya Kaunti ya Mombasa, Bi Pauline Odinga.

Bi Odinga alisema kwamba virusi havina dawa na vinafanya watoto kuwa walemavu. Aliwahimiza wazazi kuwakaribisha wahudumu wa afya ambao watakuwa wakitembea kutoka nyumba moja hadi nyingine kutoa chanjo hiyo.

“Polio husababishwa na virusi ambavyo havina dawa, mtu anaweza kupata ulemavu au kufariki. Si uchawi baadhi ya watu wanavyofikiria,” alisema.

Afisa huyo alihakikishia wazazi kwamba watoto wao watafikiwa wapatiwe chanjo akisema kwamba kutakuwa na kundi la wahudumu sita wa afya watakaotembelea nyumba zao.

Mwakilishi wa Unicef nchini Kenya, Bi Maniza Zaman alisema kwamba polio ni ugonjwa hatari kwa watoto na hawawezi kuwa salama wakikosa kuchanjwa.

“Ili kumaliza polio, watoto wote ni lazima wachanjwe. Unicef inahimiza kila familia katika maeneo yaliyoathiriwa kuhakikisha watoto wote walio na umri wa chini ya miaka mitano wamechanjwa,” alisema Bi Zaman.

You can share this post!

Muturi atawazwa msemaji Mlima Kenya

JAMVI: Wandani wauma Raila kichwa huku 2022 ikibisha hodi