Kimataifa

Watoto 700,000 wakodolea macho utapiamlo nchini Sudan

February 9th, 2024 1 min read

NA REUTERS

GENEVA, USWISI

TAKRIBAN watoto 700,000 nchini Sudan wako hatarini kukabiliwa na utapiamlo wa hali ya juu mwaka huu 2024, limesema Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) limesema Ijumaa.

Unicef imesema makumi ya maelfu miongoni mwao wanaweza kupoteza maisha.

Mapigano ya miezi 10 kati ya wanajeshi na kundi la wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) yamevuruga miundomsingi na kutumbukiza nchi hiyo katika hatari kubwa ya njaa ambapo tayari mamilioni ya watu wameingia kwa kambi za wakimbizi wa ndani na wengine nje ya nchi.

“Mojawapo ya athari za siku 300 za mapigano ni watoto 700,000 kukabiliwa na utapiamlo mbaya zaidi,” akasema msemaji wa Unicef James Elder akiwahutubia wanahabari mjini Geneva, Uswisi.

Elder alionya huenda shirika hilo lisifaulu kuwafikia watoto 300,000 ikiwa halitapigwa jeki katika juhudi zake, “kumaanisha watoto makumi ya maelfu wanaweza kupoteza maisha yao”.

Utapiamlo uliopindukia unamuweka mtoto katika hatari mara 10 zaidi kufariki endapo atakabiliwa na malaria na kipindupindu.

Alikadiria huenda watoto 3.5 milioni wakakumbana na utapiamlo wa juu.

Ili kuokoa maisha, Unicef hutoa chakula cha virutubisho vilivyo tayari almaarufu RUTF kwa watoto wanaokabiliwa na utapiamlo walio chini ya umri wa miaka mitano nchini Sudan.

Unicef inalenga kuchangisha Dola 840 milioni (kiwango sawa na Sh136 bilioni) ili kusaidia watoto zaidi ya 7.5 milioni nchini  Sudan mwaka huu 2024, lakini Elder ana wasiwasi, akilinganisha na juhudi kama hizo za miaka ya nyuma.

“Mwaka 2022 Unicef ilishindwa kufikia idadi kubwa ya watoto nchini Sudan,” akasema Elder.

Umoja wa Mataifa (UN) mnamo Jumatano ulihimiza mataifa kutowasahau raia waliojipata kwenye machafuko nchini Sudan na kuomba Dola 4.1 bilioni kwa minajili ya kufanikisha misaada ya kibinadamu na kuwasaidia wale waliokimbilia mataifa jirani.

Nusu ya raia nchini humo- karibu watu 25 milioni – wanahitaji misaada ya kibinadamu, huku watu 1.5 milioni wakiwa wamevuka na kuingia mataifa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Chad, Misri, Ethiopia, na Sudan Kusini, kwa mujibu wa UN.