Habari Mseto

Watoto 80 wanaswa kwa kutoenda shule

January 25th, 2020 2 min read

Na MISHI GONGO

WATOTO 80 walikamatwa eneo la Nyali, kaunti ya Mombasa katika msako wa kuhakikisha wote waliohitimu umri wa kwenda shule hawasalii nyumbani.

Msako huo uliokamilika Ijumaa, unaendeshwa na serikali ya kaunti na unalenga watoto walio na umri wa kati ya miaka sita hadi 18.

Akizungumza na ‘Taifa Leo’, Naibu Kamishna wa eneo hilo, Bw Henri Kipkemoi, alisema msako huo ni wa kuhakikisha kuwa serikali inaafikia mpango wa kuhakikisha wanafunzi wote wameendelea na masomo.

Bw Kipkemoi alisema msako huo ulianza Jumatatu na kukamilika jana.

“Tumeanza msako huu eneo la Matopeni ambako tulipata watoto 31 wakirandaranda. Katika eneo la kongowea tumepata watoto 20, leo tumekamilisha mitaa yote 36 katika eneo bunge hili la Mvita,” alieleza.

Bw Kipkemoi alisema msako huo umeonyesha kuwa watoto wengi hawajasajiliwa kujiunga na shule za chekechea na zile za msingi licha ya serikali kutoa pesa za kusimamia elimu yao.

“Serikali inatumia pesa nyingi kuhakikisha watoto wanapata elimu, ni hatia kwa mzazi kukataa kumsajili mtoto shule,” akaeleza.

Alisema watoto walioshikwa watapelekwa katika shule za serikali katika maeneo yao.

“Wazazi wakija kuchukuwa watoto wao, tutawaandikisha kisha kuwapeleka katika shule za serikali. Tutafuatilia kuona kuwa watoto wanapata elimu, mzazi atakayetoa mtoto wake atachukuliwa hatua,” akasema.

Bw Kipkemoi alisema eneobunge la Nyali linakumbwa na changamoto ya magenge kufuatia wazazi kukataa kupeleka watoto wao shule.

Chifu wa Kongowea, Bi Yasmin Omar alisema msako huo ulifanywa kwa ushirikiano wa wazee wa mtaa na wajumbe.

Alisema kuwa watoto wengine walipatikana wakiwa wanasaidia wazazi wao kufanya biashara katika soko la Kongowea.

“Wazazi wanakataa kuwasajili watoto shule na kuwageuza vitega uchumi, wengine wanawaweka katika biashara zao kama wasaidizi, hii ni hatia na tutawachukulia hatua,” akaeleza.

Wengi wa wazazi waliopatikana katika msako huo, walidai kuwa wamewasajili watoto wao shule japo walikuwa wamerudishwa nyumbani kufuatia kukosa bidhaa muhimu kama sare na vitabu.

“Mtoto wangu amefukuzwa kwa kukosa kulipa Sh1,000 ya huduma za shule, hata nikimpeleka atafukuzwa tena na hatuelewi hizi pesa ni za nini kama serikali imetoa pesa kwa shule hizo. Tunaomba serikali kuwaamrisha walimu kutowafukuza wanafunzi kwasababu ya pesa,” akaeleza Bi Mariam Juma.