Watoto na vijana waanza kupewa chanjo ya corona

Watoto na vijana waanza kupewa chanjo ya corona

Na MASHIRIKA

PRETORIA, AFRIKA KUSINI

AFRIKA Kusini imeanza kuwapa chanjo watoto na vijana chipukizi kama sehemu ya hatua tatu za kufanyia majaribio ya kimatibabu chanjo ya Uchina, Sinovac Biotech, kote duniani.

Chanjo hiyo dhidi ya Covid-19 inalenga watu wenye umri kati ya miezi sita na miaka 17.

Utafiti huo wa kimataifa utashirikisha wahusika 2,000 kutoka Afrika Kusini huku wengine 12,000 wakishiriki nchini Kenya, Ufilipino, Chile na Malaysia.

Kundi la kwanza la watoto kuanza majaribio hayo Afrika Kusini lilipewa dozi hiyo Ijumaa katika Chuo Kikuu kuhusu Sayansi ya Afya, cha Sefako Makgatho, katika jiji kuu la Pretoria.

Wengine watapokea dozi hizo katika maeneo sita mbalimbali kote nchini humo, Sinovac ilisema kupitia taarifa.

“Lengo kuu la utafiti huu ni kutathmini ufaafu wa dozi mbili za CoronaVac dhidi ya visa vilivyodhibitishwa vya Covid-19 kwa watoto na vijana chipukizi. Ufaafu utapimwa kwa kulinganisha watakaolazwa hospitalini na visa vya watakaougua makali ya Covid-19,” ilisema.

Kulingana na mwelekezi wa mradi huo, Sanet Aspinall, kumekuwa na “maambukizi mengi yasiyo hatari miongoni mwa watoto lakini bado wanakabiliwa na tishio.”

“Wanapata maambukizi kisha wanaweza kueneza kwa wanajamii wengine,” alisema.

Glenda Gray, rais wa Baraza la Utafiti wa Kimatibabu Afrika Kusini alisema katika hafla ya Ijumaa kwamba “kuchelewesha kuwajumuisha watoto katika majaribio ya chanjo dhidi ya Covid-19 kunachelewesha uwezo wetu wa kudhibiti gonjwa hilo.”

Kampuni za Amerika zinazounda chanjo za Pfizer na Moderna vilevile zimefanya majaribio kwa watoto hatua ambayo imefanya mataifa kadhaa kuruhusu watoto wa umri tofauti kupatiwa dozi hizo.

Afrika Kusini inajumuisha zaidi ya asilimia 35 ya maambukizi ya COVID-19 Afrika, ikiwa na visa 2.8 milioni vilivyothibitishwa, ikiwemo vifo 84,327.

Imekuwa ikipambana na kuzuka kwa mkurupuko mpya kutokana na virusi vya corona aina ya Delta huku ikiandikisha maambukizi mapya 6,270 na vifo 175 katika muda wa saa 24 zilizopita.

Watu zaidi ya milioni saba wamepokea dozi kamili za chanjo ya Johnson & Johnson inayohitaji dozi moja au Pfizer-BioNTech inayohitaji dozi mbili.

Afrika Kusini kwa sasa inatoa chanjo kwa watu wazima wote wenye umri kuanzia miaka 18 huku ikidhamiria kuwapa chanjo watu wasiopungua 40 milioni miongoni mwa raia wake 60 milioni kufikia mwisho wa mwaka.

Hata hivyo, imekuwa ikitatizika kufikia malengo yake ya kuwapa chanjo watu wasiopungua 300,000 kila siku.

You can share this post!

Wasiwasi KRA ikifunga akaunti za chuo kikuu kwa deni kuu

Rais wa Tunisia atangaza mipango ya kugeuza Katiba