Makala

WATOTO: Subira yake katika uigizaji yamvutia heri KBC

April 5th, 2018 2 min read

Na PATRICK KILAVUKA

Ndoto yake ilikuwa siku moja awe mwigizaji kwenye vipindi vya runinga kwani alikuwa mraibu wa kutazama vipindi vya michezo ya kuigiza kama Machachari na kadhalika.

Ingawa hakujua ndoto yake itafika lini, aliamini na kushikilia msemo kwamba, hayawi hayawi huwa. Ushawishi wake ulitokea pale ambapo alienda majaribio ya kipindi cha Kenda Imani cha runinga KBC na kufua dafu kusajiliwa.

Nicole Wangui, 11, ywanafunzi wa darasa saba shule ya msingi ya Visa Oshwal, Westlands huigiza katika kipindi hicho kama ‘Bela’ binti wa tajiri ambaye maisha ya kifahari yalimuathiri kimaadili licha ya kwamba, alilelewa katika mazingira ya ukristo.

Kando na hayo, humkandamiza mjakazi. Hata hivyo, ana uwezo wa kuigiza uhusika wowote kulingana na jinsi kipindi kinavyoendelea.

Alijiunga na programu hiyo ambayo hupeperusha hewani Jumatano, saa moja usiku, baada ya mama yake Faith Mucheru, zamani mwigizaji wa kipindi cha Vioja Mahakamani kumkutanisha na produsa wa kipindi Jackie Njagi Lidubwii na kumfanyia majaribio kisha akaonesha ueledi wa kuigiza uhusika uliotajwa awali .

“Ni kipindi ambacho kinaangazia stori ya kuwa na matumaini katika changamoto za maisha. Pia, kinatia moyo wajakazi kuwa na imani mambo hubadilika licha ya hali kuwa ndivyo sivyo ,” anasema “Bela” ambaye hufanya igizo za kurekodi kipindi hicho siku ya Jumamosi au likizo.

Mwigizaji chipukizi Nicole Wangui,11, mwanafunzi wa darasa saba shule ya msingi ya Visa Oshwal, Westlands ambaye huigiza shuleni na katika kipindi Kenda Imani kwenye runinga ya KBC. Picha/Patrick Kilavuka

Tayari ameshiriki katika vipindi vitano. Wangui anasema kuigiza kwenye runinga si rahisi kwani kunahitaji kujitolea sana.

Isitoshe, unafaa ujue kwamba mambo ambayo unayaangazia yanakuwa na mashiko kwa jamii na watu huwa na mtazamo chanya kuyahusu kupitia uhusika wako hali ambayo huwapelekea wengine kukosa kuelewa kwamba, hilo ni igizo tu na halina ufafanisho na tabia yako kama mwigizaji japo unachora tu taswira ya kuelimisha au kuhamasisha jamii na umma.

“Kama msanii inakubidi kukubali mtazamo wa wasikilizaji wala watazamaji ndiposa uwe na mtagusano wa rahisi nao ili watambue juhudi zako za kukuza kipawa chako na kuwa kioo cha jamii.

Pamoja na hayo, kuikomboa kutokana na  kasumba za kijamii na mienendo mibovu ambayo inachipukia. Pia, wajue kwamba mwigizaji ni mjumbe tu,” adokeza Wangui ambaye uigizaji ni fani anaipendayo na hutumbuiza.

Fauka ya hayo, anasema ukitaka kushiriki katika kurekodi vipindi, unahitajika uwe mkakamavu wakati unaporekodi na ujaribu kuigiza pasipo kufikiria kwamba unatazamwa na hadhara na ulenga kamera kimasomaso.

Wangui anakiri kwamba  kuchoka wakati mnanasa vipindi mfululizo pamoja na kumakinika kutoka mwanzo hadi mwisho kuwa changamoto ambazo anazipitia.

Miongoni mwa waigizaji ambao anawapenda ni “Joy” wa kipindi cha Machachari na Ariana Grande wa kipindi cha Victories Sam and Cat,  kutokana na ujasiri wao wakati wanapoigiza.

Manufaa? Amepata fursa ya kujiwekea hazina ya kesho kutokana uigizaji wake na hata kukutana na waigizaji wa haiba na kujifunza mengi ya fani kutoka kwao.

Kando na kuigiza, angependa kusomea udaktari usoni na wakati wa kujisawazisha, yeye huogolea na kuimba.

Mwaka huu, ana matamanio ya kushiriki katika mashindano ya Muziki na Drama ya shule za msingi kuonesha uwezo wa kipawa chake katika fani ya uigizaji.

Ushauri? Anasema uigizaji kwenye runinga, huhitaji mwigizaji kuwa mjasiri na mkakamavu, mwenye nidhamu na kujiepusha na kiburi au ujuaji wa ukwasi.