Watoto wa marais wakwama na Raila

Watoto wa marais wakwama na Raila

Na JUSTUS OCHIENG

FAMILIA za marais watatu walioongoza Kenya tangu uhuru zimeshikana kumuunga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga kuwania urais mwaka 2022.

Duru za kuaminika zimeambia Taifa Leo kuwa Rais Uhuru Kenyatta, ambaye ni mwanawe rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta amefanikiwa kushawishi familia za Daniel arap Moi na Mwai Kibaki kuunga mkono juhudi za Bw Odinga kuwa rais wa tano wa Kenya.

Wadokezi ndani ya serikali walisema familia hizo zinapasha misuli moto tayari kusukuma kampeni za Bw Odinga.

“Ingawa baadhi ya watu wa familia hizo huenda wasishiriki moja kwa moja katika kampeni, watakuwa wakiunga mkono juhudi za kuhakikisha Bw Odinga ameingia Ikulu mwaka 2022,” akaeleza afisa mmoja wa ngazi ya juu katika serikali.

Kulingana na uchunguzi wa Taifa Leo, mpango uliopo ni kubuni muungano wa vyama kadhaa vikiwemo Kanu, ODM, Jubilee na PNU miongoni mwa vingine kusimama nyuma ya Bw Odinga.

Bw Odinga amejitokeza kuwa kipenzi chao kutokana na ushawishi wake mkubwa nchini na ana uwezo wa kifedha.

Rais Kenyatta anaamini kwamba Bw Odinga ndiye kiboko cha kuzima ndoto ya Naibu wa Rais William Ruto kuingia ikulu mwaka 2022.

Mdadisi wa masuala ya kisiasa Dismas Mokua anasema kuwa familia za marais wa zamani wanaamini kuwa mali yao itakuwa salama mikononi mwa Bw Odinga.

Mbunge Maalumu wa Jubilee Maina Kamanda, Jumanne aliambia Taifa Leo kuwa Rais Kenyatta ameweka mipango kabambe ya kuhakikisha kuwa anamaliza ushawishi wa Dkt Ruto katika eneo la Mlima Kenya.

“Mpango huo umeanza kuzaa matunda na kufikia 2022 Dkt Ruto atakuwa amesalia na asilimia 20 ya wakazi wa Mlima Kenya wanaomuunga mkono,” akasema Bw Kamanda.

Rais Kenyatta tayari ametoa ishara kwamba ataunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais mwaka ujao huku akisema kwamba ushirikiano baina yao tangu Machi 2018, umemwezesha kuleta maendeleo nchini.

“Nawashukuru kwa sababu mbunge wenu wa zamani, Mzee Raila alisimama nami kuleta amani nchini. Amani hiyo imeleta maendeleo. Si mtu anayependa amani ndio mnataka. Chaguo ni lenu. Mtafanya uamuzi ufaao?” Rais Kenyatta akauliza umati uliojitokeza baada ya uzinduzi wa hospitali mbili mtaani Kibra huku akiwa ameandamana na Bw Odinga.

Rais Kenyatta alitoa ishara ya kuunga mkono Bw Odinga siku moja tu baada ya kinara wa ODM kukutana na mabwanyenye wa Mlima Kenya waliounga mkono Rais Mstaafu Mwai Kibaki wakati wa kampeni za 2002 na 2007 na Rais Kenyatta katika kampeni za 2013 na 2017.

Mjomba wa Rais Kenyatta, George Muhoho, alikuwa miongoni mwa mabwanyenye waliohudhuria mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Safari Park, Nairobi.

Jamaa mwingine wa Rais Kenyatta aliyekuwepo ni aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake wa Kiambu, Anne Nyokabi, ambaye alitangaza kuunga mkono Bw Odinga akimtaja kuwa Nelson Mandela wa Kenya.

“Baba wewe ni Joe Biden, wewe ni Mandela wetu, sisi kama wanawake tuko tayari kufanya kazi nawe tafadhali shirikiana nasi,” akasema Bi Nyokabi.

Familia ya Rais Mwai Kibaki pia imedokeza kuwa itaunga mkono Bw Odinga.

Katika mahojiano na gazeti la ‘Sunday Nation’, mwana wa Kibaki, Jimmy, alimiminia sifa tele Bw Odinga huku akisema kuwa ametoa mchango mkubwa nchini Kenya.

“..lakini nahisi kwamba anastahili kuwa rais. Namfahamu vyema, hivyo naamini kwamba anafaa kuwa rais japo sijaona manifesto yake,” akasema Bw Jimmy Kibaki.

Kuhusu Dkt Ruto, Jimmy alisema kwamba: “Sitampigia kura kutokana na sababu zangu za kibinafsi. Siamini kwamba ana sifa za kuwa kiongozi wa nchi hii.”

Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi, ambaye ni jamaa wa karibu wa familia ya Rais Mstaafu Kibaki, pia ametangaza wazi kwamba ataunga mkono Bw Odinga.

Bw Muriithi ni miongoni mwa magavana kutoka Mlima Kenya ambao wametangaza kuunga mkono Bw Odinga.

Wengine ni Francis Kimemia (Nyandarua), Lee Kinyanjui (Nakuru) na James Nyoro (Kiambu).

Afisi mkuu serikalini aliyeomba jina lake libanwe, aliambia Taifa Leo kuwa japo Rais Kenyatta hajatangaza wazi mtu atakayemuunga mkono katika kinyang’anyiro cha urais, ‘watu wanafaa kutazama ishara’.

You can share this post!

Utekaji nyara uliozidi Mlimani wazua hofu

Wavukaji feri kuendelea kulipia kupitia kwa Mpesa